MAMIA ya washiriki wamejitokeza kushiriki Nyuki Marathon ya pili iliyofanyika kwenye viwanja vya New AICC jijini Arusha, ikiwa na lengo la kuhamasisha ufugaji nyuki na kuonesha mchango wake katika uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa mbio hizo, Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo, alisema Nyuki Marathon ni zaidi ya tukio la michezo kwani inaleta ujumbe wa maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 50 wa Shirikisho la Kimataifa la Wafugaji Nyuki Duniani (Apimondia) mwaka 2027.
“Michezo kama hii inatupa fursa ya kuwaleta Watanzania pamoja, kuhamasisha ufugaji nyuki na kutuandaa kuwa wenyeji bora wa mkutano mkubwa utakaotoa fursa za kiuchumi na kijamii,” alisema Prof. Silayo huku akishukuru ushirikiano wa wadau na viongozi kutoka mataifa jirani.
Rais wa Kamisheni ya Afrika ya Apimondia, David Mukomana, alisema Nyuki Marathon ina ujumbe wa kipekee unaopaswa kuenezwa ndani na nje ya Afrika, akisisitiza umuhimu wa kulinda na kuhifadhi nyuki kama chanzo muhimu cha ajira na usalama wa chakula.
Mukomana alieleza kuwa zaidi ya asilimia 70 ya vijana barani Afrika wanahitaji ajira na ufugaji nyuki ni fursa muhimu ya kiuchumi.
Pia, aliongeza kuwa sekta hiyo inaweza kuchangia kuongeza uzalishaji wa mazao na kupunguza uagizaji wa chakula.
Rais wa Apimondia Duniani, Dkt. Jeff Pettis, alipongeza Tanzania kwa maandalizi ya mkutano huo na kueleza kuwa marathon hii ni jukwaa la kipekee la kuunganisha jamii katika kulinda bioanuai na misitu asilia.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba, alisisitiza umuhimu wa Watanzania kuunga mkono juhudi za serikali katika maandalizi ya mkutano huo na kuongeza thamani ya bidhaa za nyuki nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Workers Bee Africa, Restituta Lopes Semedo, alisema Nyuki Marathon inalenga pia kuondoa dhana potofu kuwa ufugaji nyuki ni shughuli ya watu wa kipato cha chini pekee.
“Huu ni mwamko mpya. Tunataka Watanzania waone nyuki kama hazina inayotoa asali, nta na bidhaa nyingine zenye thamani kubwa duniani. Tunawahamasisha kuzingatia viwango ili kuvutia masoko ya kimataifa,” alisema Semedo.
Mmoja wa washiriki wa mbio hizo, Miriam Kileo kutoka Arusha, alisema: “Nimefurahi kushiriki Nyuki Marathon kwa mara ya kwanza. Imenifanya nione kuwa ufugaji nyuki ni fursa ambayo hata sisi vijana wa mijini tunaweza kuichangamkia na kupata kipato.”
Marathon hiyo imewakutanisha washiriki kutoka nchi jirani zikiwemo Kenya, Zimbabwe, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, jambo linaloifanya kuwa tukio la kikanda lenye lengo la kuunganisha sauti moja ya kulinda na kuendeleza ufugaji nyuki barani Afrika.