Nitamkumbuka Mzee Ali Hassan Mwinyi kwa haya

0

Na Balozi Mbelwa Kairuki

NILIPOTEULIWA kuwa Balozi wa Tanzania Nchini China mwaka 2017 kabla sijakwenda kuripoti kwenye kituo changu cha kazi moja ya watu niliokwenda kuwaaga alikuwa Mzee Ali Hassan Mwinyi.  

Katika nasaha zake kwangu aliniambia maneno machache ambayo yalikuwa chachu katika utekelezaji wa majukumu yangu ya uwakilishi wa nchi yetu.  

Aliniambia hivi ninanukuu “unakwenda China kwa marafiki zetu wa jadi. Wenzio waliokutangulia – wameyaimarisha mahusiano yetu na Wachina kwa miaka mingi- na wewe nenda ukayaimarishe.

Lakini, ikitokea kazi ya kuyaimarisha imekushinda, basi yaache pale pale ulipoyakuta, yasirudi nyuma”… Maneno yale ndio yalikuwa yakinipa hamasa ya kufanya kazi kwa bidii zaidi ili mahusiano hayo yasirudi nyuma bali yaimarike zaidi, sikutaka kumuangusha Mzee Mwinyi.

Mwezi Novemba mwaka jana alipokuwa hapa London kwa ajili ya matibabu nilimkumbusha nasaha alizonipa mwaka 2017…. alifurahi sana kwamba nilizingatia ushauri wake, kisha akaniambia na hapa Uingereza uendelee kufanya hivyo hivyo. 

Watu wengi wamemuelezea vizuri Mzee Mwinyi alivyokuwa  jasiri, mnyenyekevu, muungwana, mzazi na mlezi. Ameelezewa pia alivyofanya mageuzi ya kiuchumi na kufungua nchi.  Mfano mmoja (close to home) ni namna alivyotoa kibali cha kufunguliwa Hospitali Binafsi ya TAG Mikocheni Hospital (ambayo hivi sasa inajulikana kama Kairuki Hospital).

Marehemu Prof. Hubert Kairuki alipata wazo la kuanzisha hospitali katika miaka ya 80 kipindi ambacho Sheria ilikuwa hairuhusu watu binafsi kuanzisha hospitali isipokuwa taasisi za dini. Prof. Kairuki aliamua kushirikiana na Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG)  ili kufanikisha azma hiyo.

Hata hivyo, watendaji ndani ya Wizara ya Afya waliokuwepo wakati huo walimshawishi Waziri wa Afya aliyekuwepo wakati huo asikubali kutoa kibali…na huo ndio ulikuwa ni uamuzi wa mwisho wa Waziri, hakutaka kusikiliza habari ya hospitali hiyo.  

Mzee Mwinyi alipata taarifa ya changamoto hiyo kutoka kwa Mpambe wake (ADC) Marehemu Colonel Thabit, ambapo alimuita Marehemu Prof. Kairuki na kumtaka amsimulie yaliyomsibu. Baada ya kusikiliza, Mzee Mwinyi alitoa idhini mwenyewe kwamba Hospitali ifunguliwe na akamuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni  Marehemu Hemed Mkali akaifungue kwani watu wa Wizara ya Afya walikuwa na kinyongo.  Shughuli hiyo ilifanyika Machi 17, 1987.

Sina shaka kwamba, kama sio Mzee Mwinyi kufanya uamuzi ule leo hii Kairuki Hospital na taasisi nyingine kama HKMU, KPIL zisingekuwepo. Funzo kubwa alilotuachia Mzee wetu Ali Hassan Mwinyi hususan wenye dhamana za kutumikia wananchi katika ngazi mbalimbali, tunapaswa kuwa  na usikivu, unyenyekevu na kutenda haki. Ubabe, umaarufu binafsi wa muda mfupi sio sifa nzuri na za kudumu kwa mtumishi wa umma.

Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Hayati Rais Ali Hassan Mwinyi Mahala Pema Peponi!

*Mbelwa Kairuki ni Balozi wa Tanzania, Uingereza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here