Nina matumaini na mabadiliko ya Sheria ya Makadhi – Dkt. Mwinyi

0

Na Subira Ally

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema, ana matumaini makubwa kuwa mabadiliko ya Sheria ya Makadhi yanayofanyika yataondoa utata pamoja na migongano ya kiutendaji katika mhimiliwa Mahakama hapa nchini.

Dkt. Mwinyi alisema hayo Ikulu Zanzibar, alipozungumza na Kamati ya Sheria mpya ya Makadhi na kupokea taarifa ya mwelekeo wa Rasimu hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti Wakili Mwandamizi wa Serikali Saleh Mbaraka.

Alisema, kutokana na dhamira njema iliyopo, ana imani kubwa kuwa sheria ijayo ya Makadhi itakuwa nzuri, yenye tija, isiyo na mivutano na yenye mwelekeo wa kujenga.

Alisema, pale rasimu hiyo itakapofikishwa katika ngazi ya Baraza la Mapinduzi, wajumbe wa Baraza hilo watapata fursa ya kuipitia, sambamba na Kamati ya sheria ya Baraza hilo kushauri juu ya vipengele vinavyofaa kuingizwa au kupunguzwa.

Dkt. Mwinyi aliwashukuru wajumbe wa Kamati hiyo kwa dhamira ya kuja na sheria mpya ya Makadhi kutokana na mahitaji yaliyopo, akibainisha hatua ya kuwashirikisha wadau itawezesha kupata mchango wa maoni ya kutosha.

Nae, Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhan Abdalla pamoja na mambo mengine alisema, kuongoza mhimili wa Mahakama, ambamo ndani yake kuna Kadhi mkuu, kunahitajika busara kubwa.

Mapema, Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria mpya ya Makadhi Wakili Mwandamizi Saleh Mbaraka, alisema lengo la sheria hiyo ni kuongeza wigo wa kutafuta haki ndani ya Mahakama za Kadhi pamoja na kuleta uharaka katika maamuzi ya kesi.

Alisema, sheria hiyo inalenga kurejesha dhana ya kuwatambua masheikh wabobezi , pamoja na kuwa na utaratibu wa kuweka Hati mbali mbali na kuweza kutumika katika Mahakama mbali mbali Duniani.
Aidha, alisema itatoa msukumo katika hati mbali mbali (ikiwemo za ndoa) kuweza kukubalika katika mataifa mbali mbali.

Wakili Mbaraka alieleza kuwa, kwa kipindi kirefu Serikali imekuwa ikipoteza fedha nyingi katika kuwasomesha Masheikh katika nchi mbali mbali Duniani ikiwemo Saud Arabia, kupitia fedha za Serikali au za wahisani, lakini matokeo yake pale masheikh hao wanaporejea nchini huachwa bila kutumika.

Alisema, kupitia sheria hiyo Masheikh hao watatambuliwa ili waweze kutoa mchango wao na kubainisha hatua hiyo itatoa ajira kwao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here