Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa ameelezea kuridhishwa kwake na Ujenzi wa Barabara ya Mabasi yaendayo haraka – (BRT) sehemu ya Katikati ya Jiji kwenda Mbagala na kumtaka mkandarasi anaejenga Barabara hiyo kuhakikisha inakamilika kama ilivyo pangwa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Prof. Mbarawa alisema katika kipindi cha miezi mitatu kutoka sasa anatarajia barabara hiyo yenye urefu wa Kilometa 20.3 itakuwa imefunguliwa yote kwa matumizi.
“Nia ya Serikali ni kupunguza msongamano Dar es Salaam, hivyo nakuagiza TANROADS na Mkandarasi kuhakikisha sehemu inayokamilika magari yaruhusiwe kuitumia wakati ujenzi unaendelea ili kupunguza msongamano na kuleta ufanisi katika huduma za usafiri na uchukuzi katikati ya jiji la Dar es Salaam,” alisisitiza Prof. Mbarawa.
Aidha, amewataka madereva wa magari katika barabara ambazo ujenzi wake bado unaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wakandarasi ili kulinda usalama wa abiria, wajenzi na magari kwa ujumla.
“…Hatuitaji ajali zitokee hivyo tutii maelekezo ya wataalam wetu yenye nia ya kupunguza msongamano na kulinda usalama wa watu na magari,” alisema Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa alisema, ujenzi wa Barabara na Madaraja jijini Dar es Salaam unafanywa kwa Awamu, hivyo wananchi waendelee kuiunga mkono Serikali ili kufikia malengo tarajiwa yaliokusudiwa.
Kwa upande wake, Meneja Mradi wa BRT, Eng. Barakaeli Mmari alisema, ujenzi wa Daraja la Juu sehemu ya Chang’ombe makutano ya barabara za Nyerere na Kawawa uko sahihi kulingana na usanifu wake, lengo ni kutoa nafasi katikati kwa magari yaendayo haraka.
Aidha, alizungumzia umuhimu wa raia wema kupata taarifa sahihi kwa TANROADS pale wanapoona katika miradi hiyo kuna jambo linalohitaji ufafanuzi.
Naye Mbunge wa Temeke, Doroth Kilave ameishukuru Serikali na kuipongeza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kutokana na kasi ya ujenzi wa miadi hiyo katika jimbo lake.
Takribani Shilingi Bilioni 262 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa Barabara ya kupunguza msongamano ya Kilwa na Daraja la Chang’ombe katika makutano ya Barabara za Nyerere na Kawawa jijini Dar es Salaam.