Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
MWAKILISHI wa Fuoni, Yussuf Hassan Iddi, amelitaka Baraza la Wawakilishi kutokuiogopa katiba na badala yake waifanyie marekebisho na kuweka muda wa Urais kuwa vipindi vitatu ili kumuwezesha Rais wa sasa Dkt. Hussein Ali Mwinyi atimize maono na ndoto zake katika kuiletea maendeleo Zanzibar.
Akizungumza wakati wa kuchangia bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Idara zake katika Baraza la 10 la Wawakilishi, Mkutano wa 19, Kikao 01 Mjini Zanzibar, mwakilishi huyo alisema Katiba sio msahafu, ndio maana ilifanyiwa marekebisho mara mbili kuruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992.
Alisema, mwaka 2010 yalifanyika mabadiliko ambayo yaliunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na uamuzi huo unawezekana kwani katika Kifungu cha Katiba 80 (2) kinaeleza hatua za kufuata pale kunapohitajika mabadiliko ya katiba ikiwa ni pamoja na kuitisha kura za maoni.
“Mimi nasema leo tukiitisha kura za maoni katika wilaya zote 11 za Zanzibar zaidi ya asilimia 80 ya wananchi watasema wanataka aendelee,” alisema mwakilishi huyo Yussuf Iddi na kuongeza kuwa Rais mwenye maono na ndoto kubwa kama Dkt. Hussein Ali Mwinyi kumpa miaka 10 ni kukatisha ndoto zake ni vema mabadiiliko yakafanyika na muda wa kufanya hivyo ni sasa.
Alisema, kipindi cha miaka 10 ni kifupi na kuongeza, ukomo wa Urais utaipunguzia Serikali gharama kubwa inazotumia kwa wastaafu na anasema hata watangulizi wake waliondoka bila kutimiza maono na ndoto zao kwa nchi yao.
“Kipindi cha miaka 10 kifupi kinazalisha viongozi wastaafu wengi, Serikali inapata mzigo mkubwa wa kuwahuduma huku inasubiri Rais anayekuja baada ya kumaliza muda wake” alisema Mwakilishi huyo.
Alisema, wote waliomtangulia Dkt. Hussein walikuwa na ndoto lakini ukomo wa Urais ukawafanya washindwe kuzifikia na ni vema tukaenda na vipindi vitatu badala ya viwili,” alisema na kuongeza kuwa kwa aliyoyafanya Zanzibar hadi hivi sasa, hakuna mgombea anayeweza kusimama nae Oktoba katika Uchaguzi Mkuu akaambulia kitu.