Msajili Hazina: Ni wakati wa Tanzania kunadi fursa za uwekezaji Kimataifa

0

KATIKA jukwaa kubwa la viongozi wa taasisi za kibiashara barani Afrika, maarufu kama Africa CEO Forum, Tanzania imeendelea kujidhihirisha kama taifa linalochomoza kwa kasi kiuchumi na kuvutia uwekezaji wa kimataifa.

Mkutano huo wa siku mbili ulioanza Jumatatu, Mei 12, 2025, Abidjan Ivory Coast, na kuhudhuriwa na zaidi ya maafisa watendaji wakuu, wawekezaji na viongozi wa taasisi za sekta za umma wapatao 2,000 kutoka nchi zaidi ya 75, uligeuka kuwa jukwaa muhimu kwa Tanzania kuonyesha mafanikio yake, mikakati ya maendeleo, na dhamira ya kujenga uchumi wa kisasa unaoshirikisha sekta binafsi kwa karibu.

Katika msafara ulioongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, pamoja na viongozi wengine wakuu akiwemo Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, Tanzania iliwasilisha taswira mpya ya taifa linalofungua milango yake kwa wawekezaji wa ndani na nje, huku ikitangaza mageuzi makubwa ya kiuchumi yanayoendelea nchini.

“Kikao chetu cha leo (jana-May 12) kikiwa na wawekezaji zaidi ya 2,000 ni nafasi adhimu kwetu kuwavutia, kuchukua mawazo yao na kuwafanya waijue Tanzania yetu,” alisema Mchechu, akisisitiza nafasi ya kipekee ambayo Tanzania imejijengea katika jukwaa hilo la kimataifa.

“Nchi zote zinapigania nafasi za kiuchumi. Tanzania kwa sasa ina mtaji mkubwa kutokana na msingi wa mahusiano na sera za kiuchumi zinazowekwa na viongozi wetu.”

Kwa mujibu wa viongozi wa Tanzania, vikao vya Africa CEO Forum si tu sehemu ya kujifunza, bali ni jukwaa la kuuza fursa za kiuchumi za Tanzania, hasa katika maeneo ya logistiki, madini, kilimo na fedha. Wameeleza kuwa ni muhimu kwa Tanzania kuendelea kushiriki kwa bidii katika majukwaa haya ili kuwa mhimili wa mijadala ya maendeleo Afrika.

“Tunaamini kupitia mkutano huu, dunia inazidi kuijua Tanzania – sio tu kama nchi yenye utulivu wa kisiasa, bali kama taifa la fursa, la watu wenye vipaji, na la mazingira rafiki kwa biashara,” aliongeza Mchechu.

Mjadala mkuu wa mkutano huo ulilenga kuangalia namna bora ya kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.

Katika hili, Waziri Mkuu Majaliwa alieleza kwa kina jinsi Tanzania ilivyofanikiwa kufungua fursa za uwekezaji kwa kushirikiana kwa karibu na taasisi kama Shirikisho la Sekta binafsi Tanzania (TPSF) na Shirikisho la wenye viwanda Tanzania (CTI).

“Tanzania ni nchi inayoendelea kufungua milango kwa sekta binafsi – ya ndani na ya kigeni – kuwekeza. Ushirikiano huu unasaidia kuongeza uwezo wa uchumi wa ndani, na kuchangia huduma za kijamii kwa wananchi kupitia mapato ya Serikali,” alisema Waziri Mkuu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here