MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hammad Abdallah, ameendelea kufuatilia kwa karibu miradi mikubwa ya Shirika, ambapo leo amefanya ziara kwenye mradi wa Samia II Medeli, Dodoma.
Ziara hiyo ililenga kujionea kasi na ubora wa ujenzi ambao unaendelea kwa kiwango cha kuridhisha.
Akiwa ameambatana na Meneja wa NHC Mkoa wa Dodoma, Gibson Mwaigomole, Abdallah alipata fursa ya kushuhudia mafundi na wahandisi wakihakikisha kila hatua ya ujenzi inakwenda kwa mpangilio.
Miongoni mwa shughuli zilizokuwa zikiendelea ni kumwagilia tofali zilizotengenezwa, kufanya usafi wa eneo la mradi, pamoja na kazi ya curing ya Raft Foundation za Block M na N na foundation wall za Block K, M na N.
Kadhalika, ujenzi wa foundation wall za Block M na N umeendelea kwa umakini mkubwa huku zaidi ya tofali 1,500 za inchi 5 zikitengenezwa kwa uwiano sahihi wa 30 kwa kila mfuko wa saruji, tayari kwa maandalizi ya superstructure.
Aidha, timu ya ujenzi imefanikiwa kusimika lift shaft shuttering na formwork za starter columns za Block M, jambo linalothibitisha nidhamu ya kazi na uthabiti wa usanifu.
Mradi huu wa kisasa unatarajiwa kuongeza fursa kubwa za makazi na biashara katika Jiji la Dodoma, sambamba na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wake.
Hatua hii inaonyesha dhamira ya NHC kuendeleza miradi ya kimkakati itakayosaidia kufanikisha azma ya serikali ya kujenga makazi bora na ya kudumu kwa Watanzania.