MWENGE wa Uhuru umeendelea kuleta matumaini kwa wananchi baada ya kuzindua mradi mkubwa wa maji safi na salama wenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.494 katika Vijiji vya Kwala na Mwembe Ngozi, unaotarajiwa kuwahudumia wakazi 6,407 wa maeneo hayo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.
Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Kibaha, Mhandisi Debora Kanyika, alisema mradi huo ni matokeo ya maombi ya wananchi waliokuwa wakikumbwa na adha kubwa ya upatikanaji wa maji kutokana na uchakavu wa miundombinu ya zamani iliyojengwa mwaka 1974.
“Awali wananchi walilazimika kununua ndoo moja ya maji kwa Shilingi 300 kutoka kwa magari ya kubeba maji, hali iliyosababisha mzigo mkubwa wa kiuchumi kwa familia nyingi,” alisema Mhandisi Kanyika.
Alieleza kuwa baada ya utekelezaji wa mradi huo, wananchi sasa wanapata maji safi kwa gharama ya Shilingi 40 kwa matumizi ya nyumbani na shilingi 50 kwa matumizi ya viwandani.
Mradi huo kwa sasa unasimamiwa na chombo cha maji ngazi ya jamii kinachojulikana kama Minazimikinda CBWSO.
Chanzo cha maji ya mradi huo kiko Kijiji cha Minazi Mikinda na kinatokana na kisima chenye urefu wa mita 33 chenye uwezo wa kutoa lita 43,000 kwa saa.
Mhandisi Kanyika alisema, mkataba wa mradi ulisainiwa Machi 2022 na kukamilika Aprili 2024. Hivi sasa mradi upo katika kipindi cha matazamio hadi mwisho wa mwezi huu.
Katika ujenzi wake, wananchi 100 walinufaika kwa kupata ajira za muda, huku ajira za kudumu 10 zikiwa zimepatikana.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ussi, alipokuwa akizindua mradi huo aliwataka wananchi kulinda miundombinu ya maji ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuwanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.
Wakazi wa Minazimikinda, Salma Mohamed na Zainab Hussein, walieleza furaha yao kwa Serikali kwa kuleta mradi huo ulioondoa usumbufu mkubwa waliokuwa wakikumbana nao kila siku.
“Awali tulitumia muda mrefu kutafuta maji, lakini sasa tunaweza kutumia muda huo kufanya shughuli nyingine za maendeleo,” alisema Salma kwa furaha.