Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha BNU (Beijing Normal University) na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wamezindua mradi utakaowezesha wasichana na wanawake katika nyanja za sayansi, uhandisi na hisabati.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo ambao umefanyika Machi 14, 2025 Jijini Dodoma Mkurugenzi Elimu Msingi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Abdul Maulid Mnonya aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo alisema, mradi huo utachochea kupata wataalam katika kukuza maeneo ya sayansi na kompyuta nchini.

Alibainisha kuwa, Serikali itaendelea kusaidia jinsia ya kike katika ukuaji wa Teknolojia ya Kidijitali nchini kwani kundi hilo lilikuwa limeachwa nyuma.
“Niwapongeze UNESCO na Chuo kikuu cha BNU, kwa kuleta mradi huu nchini, utakaowezesha mafunzo kwa wasichana na Wanawake katika mafunzo yao ya Kidijitali.
Mradi huu ni mpango wa kidijitali kwa wasichana na wanawake, ambapo Serikali wameuchukua na kuuweka katika mpango wa kimaendeleo na sera ya elimu hapa nchini, hivyo tunaendelea kuwapongeza wadau kwa kushirikiana nasi katika kusaidia jinsia ya kike,” alisema.
Aidha, alisema mradi huo utaenda katika mikoa yote, kwenye vyuo vyote vya elimu na maeneo ya elimu nchini.

Aliongeza kuwa, utakuwa chachu kubwa kwani takwimu upande wa wasichana na wanawake ni asilimia 30 chini ya wavulana na wanaume.
“Kwa upande wa kisayansi wasichana na wanawake waliachwa nyuma, hivyo lengo la mradi huu ni kupandisha kutoka kiwango hicho na kupata uwiano sawa.
Kwa kutambua hilo, Serikali iliweka malengo katika mipango ya miaka 50, kwa kuingiza sera yake kwenye elimu kwa wanawake kidijitali,” alisema Abdul Mnonya.
Akihitimisha wakati wa ufunguzi huo alisema, Serikali itaendeleza mradi huo hata utakapokwisha kwani ni wa muhimu. “Mradi huu wa miezi 26 kwa maana ya miaka miwili, Serikali tunaahidi na hata ukiisha, tupo tayari kuuendeleza.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa UNESCO nchini Tanzania, Michel Toto ametoa shukrani zake kwa Chuo cha BNU na Serikali ya Tanzania kwa mradi huo kwani utatoa nafasi kwa jinsia ya kike kuyaelewa masomo ya Sayansi ili kuwasaidia katika mapambano ya ukuaji wa Teknolojia duniani.
Nae Msimamizi Mkuu wa mradi huo kutoka UNESCO Dkt. Una McCarthy-Fakhry alisema, wanatarajia mapinduzi makubwa kupitia mradi huo ambao pia unatekelezwa nchini Ghana, ambapo UNESCO wameona umuhimu wa kumsaidia msichana na Mwanamke katika Teknolojia na dijitali.
