Mradi wa JNHPP wakamilika rasmi

0

đź“Ś Watajwa kuikomboa Tanzania kiuchumi

đź“Ś Dkt. Biteko awapongeza waandishi wa habari kuhabarisha umma mradi wa JNHPP

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuwa kinara kufuatia jitihada zake za kukamilisha utekelezaji wa mradi wa Kufua Umeme wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115.

Hayo yameelezwa leo Aprili 5, 2025 Rufiji mkoani Pwani na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko mara baada ya kutembelea mradi huo.

“Tunamshukuru sana Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukamilisha kutekeleza mradi huu ambao ulikuwa umefikia asilimia 30 wakati anaingia madarakani, kupitia uongozi wake aliweka mkakati mzuri uliosaidia kukamilisha mradi huu,” alisema Dkt. Biteko.

Alisema kuwa, mradi huo sasa umekamilika na una mitambo tisa itakayotumika kwa ajili ya kuzalisha umeme.

Aidha, amewashukuru wakandarasi kutoka Kampuni ya Arab Contractors na wataalamu kutoka Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) kwa kukamilisha mradi kwa weledi na viwango vizuri.

Amewahakikishiwa Watanzania kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Samia ipo tayari kuhakikisha Watanzania wanapata umeme wa uhakika na inaendelea kujenga vyanzo vipya vya kuzalisha umeme nchini.

Amebainisha kuwa tayari Serikali imetoa shilingi trilioni 6.5 ikiwa ni gharama ya ukamilishaji wa mradi huo wa JNHPP.

Pamoja na hayo, Dkt. Biteko amevishukuru ma kuvipongeza vyombo vya habari nchini kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuhabarisha umma kuhusu utekelezaji na mafanikio ya miradi mbalimbali ya Serikali ikiwemo mradi wa JNHPP.

“Waandishi wa habari mliibeba ajenda hii ya Taifa, katika vyombo vyenu vya habari na kwa kweli vina mchango mkubwa. Naomba mnifikishie shukrani zangu kwa wahariri na wakuu wa vyombo vyenu vya habari kwa kuhabarisha umma na kuna wakati hata kwa kutoa ufafanuzi wakati ambao tulihitaji wananchi wapate taarifa kamili na zenye usahihi,” alisisitiza Dkt. Biteko.

Katika hatua nyingine, ameipongeza TANESCO na TECU kwa kukamilisha mradi kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amesema kukamilika kwa mradi huo ni ukombozi wa kiuchumi.

Naye, Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Hamadi Masaun amesema Tanzania imeingia katika historia barani Afrika ambapo alisema, kazi kubwa iliyobaki ni kutunza vyanzo vya maji ili kuulinda mradi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here