Mkakati wa ukusanyaji wa mapato wa miaka mitatu wazinduliwa

0

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, amezindua Mkakati wa Muda wa Kati wa Ukusanyaji wa Mapato wa Miaka Mitatu (Medium Term Revenue Strategy) uliopangwa kutekelezwa kuanzia mwaka 2025/2026 hadi 2027/2028 na Kamati za usimamizi na utekelezaji wa Mkakati huo.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mkakati huo, ukumbi wa Kambarage Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma, Dkt. Mwamba alisema kuwa Mkakati huo unalengo la kuweka msingi imara ya ukusanyaji wa mapato, kuweka utabirifu wa sera za mapato na kuongeza makusanyo ya mapato.

Alisema kuwa utekelezaji wa Mkakati huo utasaidia kuongeza uhiari wa ulipaji kodi, kutambua na kuziba mianya ya ukwepaji kodi, kupunguza nakisi ya bajeti na kuimarisha imani ya wananchi na uwekezaji katika mfumo wa mapato.

“Utekelezaji wa kazi hii utaboresha usimamizi wa mapato ya Serikali na kuhakikisha tunakuwa na bajeti endelevu itakayowezesha Serikali kuongeza kasi ya utoaji wa huduma muhimu kwa wananchi kwa kutumia mapato ya ndani”, alisema Dkt. Mwamba.

Dkt. Mwamba alisema kuwa Mkakati umeainisha maboresho ya mikakati na hatua mbalimbali ambazo zimekuwa zikiendelea kutekelezwa na Serikali katika kuhakikisha Serikali inakusanya mapato mengi kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani.

Alisema kuwa hatua hizo zimegawanyika katika makundi matatu ambayo ni mapendekezo ya maboresho ya sera, maboresho ya usimamizi wa ukusanyaji wa mapato na maboresho ya Sheria.

Dkt. Mwamba alisema kuwa Mkakati huo ulioandaliwa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo washirika wa maendeleo na wadau wengine kutoka taasisi za Serikali na sekta binafsi, unapendekeza kuandaliwa kwa sera ya kodi kitaifa itakayotoa mwongozo wa kuandaa na kuboresha sera za kodi na kuboresha mifumo ya kielektroniki inayotumika katika ukusanyaji wa mapato.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here