KAMATI ya Fedha na Uongozi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha imefanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi Milioni 873.8 inayotekelezwa katika wilaya hiyo.
Miradi iliyotembelewa ni pamoja na ujenzi wa jengo la utawala katika Shule ya Sekondari Milalanzi, ujenzi wa jengo la kuhifadhia maiti katika Kituo cha Afya Magindu, ujenzi wa Kituo cha Afya Ruvu, uendelezaji wa Hospitali ya Wilaya ikiwemo ununuzi wa vifaa tiba, pamoja na ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na matundu sita ya vyoo katika Shule ya Msingi Uhuru.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Shomari Minshehe, amesema mikopo ya asilimia kumi inayotolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu imechangia kuanzishwa kwa miradi ya kiuchumi na kuongeza ajira.
Ameeleza kuwa kupitia mikopo hiyo, kikundi cha vijana cha Mujore kimeweza kuendeleza mradi wa zahanati baada ya kupatiwa mkopo wa Shilingi Milioni 30, fedha zilizotumika kununua vifaa tiba ikiwemo mashine za Full Blood Picture, Chemistry Analyzer, Urine Analyzer, Microscope pamoja na dawa.
Aidha, Minshehe ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha ununuzi wa vifaa vya mazoezi ya tiba (physiotherapy) katika Hospitali ya Wilaya ya Kibaha, huduma ambayo haikuwepo hapo awali.
Amesema hatua hiyo imeondoa adha ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo na imeongeza upatikanaji wa huduma za afya ndani ya wilaya.
Pia , Kamati hiyo imekagua pia mradi wa kikundi cha wanawake cha Engutoto kilichowezeshwa kwa mkopo wa shilingi milioni 30 kwa ajili ya kuanzisha kiwanda cha kufyetua tofali.
Minshehe ameipongeza Idara ya Afya chini ya Mganga Mkuu, Wilford Kondo, kwa usimamizi mzuri wa miradi ya afya na kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Regina Bieda, kwa usimamizi na ufuatiliaji wa miradi pamoja na utekelezaji wa mikopo ya asilimia kumi, huku Madiwani wakiridhishwa na miradi yote iliyotembelewa.