‘Mfumo wa NeST unafanya vizuri kuliko yote Afrika Mashariki’

0
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dennis Simba, akizungumza katika kikao kazi na wahariri na waandishi wa vyombo ya habari nchini, kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR). Kilichofanyika Novemba 4,2024 Jijini Dar es Salaam.

MFUMO mpya wa Kielektroniki wa manunuzi ya Umma (NeST- National – e – Procurement System) ambao ulianza kutumika rasmi nchini Julai 1, 2023 unafanya vizuri kuliko mifumo yote Afrika Mashariki.

Mfumo huo ni mbadala wa mfumo wa awali wa manunuzi ya Umma uliojulikana kama Tanzania National e Procurement System (TANePS) na umeanzishwa kwa ajili ya kuongeza uwazi, kuongeza usalama wa taarifa na wigo wa ushiriki, kuongeza uwajibikaji, kupunguza mianya ya rushwa, urahisi wa upatikanaji wa taarifa na kupunguza muda wa mchakato.

Afisa Mwandamizi wa Habari na Mawasiliano kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina Sabato Kosuri,

Akizungumza hivi karibuni jijini Dar es Salaam na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kwenye kikao kazi kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR), Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa UMMA (PPRA) Dennis Kwame Simba alisema, uanzishwaji wa mfumo huo ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambayo iliweka wazi kuhusu suala la kutumia TEHAMA katika ununuzi wa umma.

“Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ambayo ni ahadi yake kwa kipindi cha miaka mitano, moja kati ya ahadi zake ni matumizi ya teknolojia ya TEHAMA katika kurahisisha ununuzi wa umma na kuweka usimamizi,” alisema Simba.

Aliongeza kuwa, mfumo huo ni bora na kuthibitisha hilo, Tanzania kupitia PPRA wamealikwa kufanya wasilisho kuhusu utendaji wa mfumo wa NeST, kwenye mkutano wa taasisi za ununuzi wa umma Afrika unaotarajia kufanyika hivi karibuni Kigali nchini Rwanda.

Alisema, kutokana na mfumo huo, yamejengwa mazingira wezeshi kwa ajili ya ununuzi wa umma na nchini inapata maendeleo makubwa kutokana na usimamizi mzuri uliopo hususani unaofanyika kupitia teknolojia za kisasa.

Meneja wa Kanda ya Pwani wa  PPRA Vicky Mollel

“Katika kipindi cha Awamu tatu au nne zilizopita tumeona kasi kubwa ya maendeleo, kwa kipindi kifupi tunaweza kuwa ndio Taifa linaloongooza ndani ya Afrika Mashariki, yote ni kwasababu ya umakini wa Serikali, umakini wa Wizara ya Fedha, na taasisi kama za kwetu zinazosimamia miradi na inatekelezeka,” alisema Simba.

Aliendelea kusema, “Tunafahamu changamoto kwenye nchi mbalimbali za Afrika, kuna miradi haitekelezeki inaanza na kuishi kati, kwa kutumia taasisi kama yetu, ndani ya Afrika Mashariki tuna treni ya kwanza inayotumia umeme, ni suala kubwa, tumekuza Shirika letu la ndege, tumeweka uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu”

Aidha, Simba alisema katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuhakikisha huduma zinapatikana kwa urahisi, wameweka ofisi za Kanda na wanafanyakazi kuanzia ngazi ya Kata na wanafika kwenye Kanda zote.

Awali, akizungumzia kuhusu malengo ya kuanzishwa kwa PPRA, Mkurugenzi Mkuu huyo alisema, sheria ya manunuzi ya umma sura Na. 410, imeunda Mamlaka hiyo ili kuhakikisha upatikanaji wa thamani ya fedha katika ununuzi na ugavi.

Alisema, lengo jingine ni kuhakikisha uzingatiaji wa haki, ushindani, uwazi, uendelevu, uwajibikaji, matumizi mazuri ya fedha, ufanisi na uadilifu katika ununuzi na ugavi, pia kuweka viwango vya mifumo ya ununuzi wa umma na ugavi.

“Malengo mengine ni kuhakikisha taasisi nunuzi zinatoa upendeleo kwa wazabuni wa ndani katika zabuni za bidhaa, kazi za ujenzi na huduma, pia kufuatilia uzingatiaji wa sheria kwa taasisi nunuzi na kujenga uwezo katika ununuzi na ugavi,” alisema Simba.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile aliwapongeza PPRA kwa kurahisisha mfumo wa ununuzi, huku akiwasihi wamiliki wa vyombo vya habari kujiunga na mfumo huo, kwani hata matangazo ya kwenye vyombo vya habari mengi yanapitia huko.

“Sisi tunaoendesha vyombo vya habari kama huna akaunti ya NeST huwezi kufanikisha matangazo, hali ngumu ya vyombo vya habari tuliyonayo tuna nafasi ya kujikomboa kupitia kwenye mfumo huu,” alisema Balile.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF) Deodatus Balile 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here