Meli za mizigo zaongezeka Bandari ya Tanga

0

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian amesema maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali katika Bandari ya Tanga yameongeza uwezo na ufanisi wa bandari hiyo katika kuhudumia meli na shehena.

Alisema, idadi ya meli zinazotia nanga kwa ajili ya kushusha na kupakia shehena imeongezeka kutoka 198 mwaka 2021 hadi meli 307 mwaka 2025.

Balozi Batilda alisema hayo Jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO kuelezea mafanikio ya Mkoa huo katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Alisema, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Katika kipindi cha mwaka 2020 hadi Aprili 2025 imetekeleza mradi mkubwa wa kimkakati wa maboresho ya bandari hiyo kwa awamu mbili ambapo Jumla ya Shilingi Bilioni 429.1 zimetumika.

Balozi Batilda ameeleza kuwa kufuatia maboresho hayo shehena (mizigo) imeongezeka kutoka tani 888,130 mwaka 2021 hadi tani 1,191,480 zinazopakuliwa na kupakiwa kwenye makasha (TEUS) kupitia bandari hiyo kutoka 7,036 hadi makasha 7,817 ambapo pia muda wa kuhudumia meli umepungua kutoka siku 5 hadi siku 2.

Katika hatua nyingine Balozi Batilda Burian alisema, Mkoa wa Tanga umepokea Shilingi Trilioni 1.118 kwajili ya ukarabati mkubwa wa kivuko cha MV Tanga ili kusaidia wananchi kupata huduma hiyo kwa urahisi zaidi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here