WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, ameagiza tathmini ifanyike kubaini maeneo ambapo wanafunzi wanalazimika kusoma chini au kukaa chini ya miti.
Pia, amewataka wakurugenzi wa halmashauri na wataalamu wao kuandikiwa barua za kujieleza juu ya hali hiyo.
Agizo hilo limetolewa leo, Februari 13, 2025, jijini Dodoma, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kukabiliana na msongo wa mawazo kazini kwa watumishi wa TAMISEMI.
Mchengerwa alisisitiza kuwa, haiwezekani katika karne hii wanafunzi wakakosa madarasa au madawati, ilhali Serikali imetumia matrilioni ya shilingi kuboresha sekta ya elimu.
“Miaka yote tumekuwa tukipata usumbufu ikifika Desemba na Januari, lazima zitafutwe Shilingi Bilioni 250 au 300 kwa madarasa na madawati. Lakini sasa miaka miwili imepita hatujamuomba Rais fedha za kujenga madarasa au kununua madawati. Msisubiri msukumwe, fanyeni kazi,” alisisitiza Mchengerwa.
Mchengerwa alitumia nafasi hiyo kutoa agizo kwa Idara ya Usimamizi wa Elimu ya TAMISEMI kufanya tathmini ya shule zote za msingi na sekondari zilizo chakavu ili kuweka mpango wa ukarabati.
Aidha, aliwapongeza watumishi wa TAMISEMI kwa kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa ufanisi na kuwataka kuendelea kutoa huduma bora zinazokidhi matarajio ya wananchi.
Kuhusu sekta ya afya, Mchengerwa ameeleza kuwa juhudi za TAMISEMI zimechangia kupunguza vifo vya mama na mtoto, huku akihimiza ufuatiliaji wa karibu kwa waganga wakuu wa mikoa na wilaya ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Waziri Mchengerwa amewahimiza watumishi hao kuwafuatilia kwa karibu Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya na kwenye vituo vya afya ili waongeze kasi ya kuwahudumia wananchi kwa weledi.