Na Cletus Sanga, WAF – Dar es Salaam
WAZIRI wa Afya, Mohamed Mchengerwa, ameweka mkazo mkubwa katika kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya,huku utoaji wa huduma hizo ukizingatia misingi thabiti na maadili.
Mhe. Mchengerwa amesema hayo leo, Aprili 2, 2026, wakati wa kikao kazi na wadau wa sekta ya afya kilichoambatana na ziara ya kutembelea Bohari ya Dawa (MSD), jijini Dar es Salaam.
Waziri Mchengerwa amesema kuwa Serikali inaendelea kufanya juhudi mbalimbali katika kuhakikisha huduma za afya zinaimarika na kusogezwa karibu na wananchi, jambo linalorahisisha upatikanaji wa huduma hizo.
Mchengerwa, ameongeza kuwa, uwekezaji katika miundombinu na rasilimali watu umeendelea kuimarishwa, jambo linalosaidia kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa.
Utoaji wa huduma bora zinahitaji wataalamu waliokamilika na vifaa vya kisasa, na serikali inaendelea kuhakikisha haya yanapatikana.
Aidha, Waziri Mchengerwa amesema Serikali imeendelea kusisitiza haki ya kila mwananchi kupata huduma bora kwa wakati unaofaa, jambo linaloongeza imani wananchi katika Sekta wa afya hapa nchini.