Mchango wa mwanamke katika siasa na uongozi wa Jamii

0

Na Sheikh Kamal Abdul-Mu’ty Abdul-Wahed – Al Azhar University

KUSHIRIKI katika shughuli za kisiasa ni juhudi anazozifanya mtu kwa kujitolea akishirikiana na wengine katika jamii yake.

Kwenye ushiriki huo wanajamii hushiriki kuwachagua viongozi wa ngazi mbalimbali kuanzia ngazi ya chini hadi ya Kitaifa.

Ushiriki huo unawezekana kuwa wa njia iliyo moja kwa moja au isiyo moja kwa moja, kwa lengo la kuunda sera kuu ya nchi, na kuangalia namna ya kuitekeleza. 

Wanawake ni miongoni mwa wanajamii wanaoshiriki kikamilifu kwenye michakato hiyo ya kisiasa kama ilivyo kwenye shughuli nyinginezo za kijamii.

Dini hazioneshi kuwa na tatizo na ushiriki huo; mathalan Dini ya Kiislamu inakokoteza jambo hilo, cha muhimu mipaka iliyowekwa na Mola Muumba izingatiwe, na kila mtu atekeleze wajibu wake bila kuathiri maumbile yake au jinsia yake.

Kwa kweli, mwanamke katika enzi mbalimbali alikuwa na shida maalumu, ambazo zinatofautiana kutoka wakati mmoja hadi mwingine, na kutoka nchi moja mpaka nyingine.

Lakini, mwanamke katika enzi ya Mtume (S.A.W), yaani miaka 1400 iliyopita (karne ya Saba) au mika takriban 500 baada ya Yesu Kristo/Nabii Issa A.S), hakuwa na shida yoyote, wala katika enzi ya Makhalifa waongofu, wala hata katika enzi yoyote yenye kutegemea utawala wa Qur’aan na Sunna (Mwenendo wa maisha ya Mtume Amani ya Mola iwe Juu yake).

Wanawake katika enzi ya Mtume (S.A.W) walikuwa wanafanya kazi, lakini kazi ya wanawake katika Uislamu huwa na vidhibiti mahususi vya kuhakikisha kuaminika na kujiweka mbali na fitina na kuiihifadhi jamii nzima.

Kazi zilizokuwa zinashughulikiwa na mwanamke katika enzi hiyo ziko katika aina nne:- Kwanza, Kazi za matibabu; Wanawake walikuwa wanawasaidia wanajamii na hata wanajeshi vitani kwa ajili ya kuwatibu majeruhi na kuwahudumia.

Pia, walikuwa wanatayarisha chakula kwa majeshi vitani kama ilivyosimuliwa katika Hadithi ya Mwanamama Umm Attiya (R.A) kwamba; “Nilishiriki katika vita pamoja na Mtume (S.A.W) vita saba, ambapo nilikuwa nawahifadhia wapiganaji mizigo yao (ikiwemo kuhifadhi silaha kwenye maghala), kuwaandalia chakula, kutibu majeruhi (madaktari) na kuwasaidia wagonjwa (wauguzi)”.

Pili, Kazi za kilimo; Wanawake walikuwa wakijihusisha na kilimo cha aina mbalimbali kwa ngazi zote kuanzia ngazi ya utayarishaji shamba hadi uvunaji; vivyohivyo kwenye ufugaji.

Tatu, Kazi za mikono; Imesimuliwa kutoka kwa mke wa Swahaba Bwana Abdullah Bin Masoud (R.A) kwamba, enzi za Mtume (S.A.W) wanawake walikuwa wanatengeneza vitu vya nyumbani ili kusaidia waume zao kuendesha maisha yao, kwa hiyo walikuwa wakifanya kazi mbalimbali za Mikono.

Nne, Wanazuoni wa Dini; Kazi ya kutoa fatwa na mafundisho ya Dini inajulikana sana katika sira (historia) ya maswahaba wa kike, wakiwemo wake za Mtume (S.A.W) kama vile Bi Aisha (R.A) na Umm Salama (R.A), bali pia Mtume (S.A.W) alikuwa anawaombea shauri baadhi ya wake zake katika masuala mbalimbali.

HITIMISHO

Kwa kweli Uislamu umeainisha masharti maalum kwa kazi za mwanamke ambazo ni pamoja na kuwepo kwa udharura ya kazi hizo, au kuwa jamii inahitaji kazi hiyo toka kwake.

Pia, miongoni mwa masharti ya kumruhusia mwanamke afanye kazi ni ‘kutowachanganya’ wanaume, kazi aifanyayo iambatane na maumbile ya mwanamke, iafikiane na hali ya mwanamke aliyonayo, na kuomba ruhusa ya kufanya kazi kutoka kwa Mumewe (kama kaolewa) au Walii wake yeyote (kama hajaolewa). 

Vilevile, kati ya masharti ya mwanamke kuruhusiwa kufanya kazi ni kuwajibikia Hijabu (ajihifadhi kwa maana zote za kujihifadhi) iwe mavazi yanayokubalika au utu wake; na kutosafiri ila kwa idhini ya mumewe, na anaposafiri awe mwenye kumhifadhi (mumewe) yaani asitoke nje ya ndoa, na halkadhalika kazi hiyo isimsabibishie kupoteza haki alizomfaradhishia Mwenyezi Mungu Mtukufu, (yaani haki za lazima mbele ya mumewe na wanawe).

Kwa kuchambua haki na wajibu za mwanamke katika Uislamu tunatambua kuwa, msingi wa hayo yote ni kumtunza mwanamke na kumheshimu nafasi yake, hadhi yake na utu wake katika jamii.

Pia tunatakiwa kutambua kwamba, mwanamke ana mchango muhimu sana na mkubwa mno wa kujenga jamii na nchi, kuanzia nyumba ya baba yake (akiwa Binti) au mume wake (akiwa mke, mama, na mwalimu wa kwanza wa kila mtoto Duniani), kisha mshauri na mtendaji katika nyanja mbalimbali za kazi na shughuli tofauti za maisha.

Kwa hiyo majukumu ya mwanamke katika Uislamu hayahusishwi kwa shughuli za nyumbani tu, bali anatakiwa kuwa na mchango wake katika jamii bila ya kuathiri kazi zake za msingi alizopewa na Mola wake. 

*Mwandishi wa Makala hii ni Msomi bobezi wa Elimu jamii toka Chuo Kikuu kikongwe Duniani cha Al-Azhar Sharif kilichoko Cairo nchini Misri, na Mwanachama wa Kituo cha Kiislamu cha Misri Dar es Salaam, Tanzania. Email: eg_islamic39@yahoo.com_center.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here