Na Mwandishi Wetu, Dodoma
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema Wajumbe wake wa Mkutano Mkuu wa Taifa, wanaondoka katika Jiji la Dodoma huku wakiwa wamebeba matumaini ya kupata ushindi kuliko wakati wowote.
Mamia ya Wajumbe hao toka Mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar wameliacha Jiji Kuu hilo la Tanzania ,wakiamini chama chao kitashinda uchaguzi Oktoba Mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Katibu wa Kamati Maalum yya NEC Zanzibar, Idara ya itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamsi Mbeto Khamis, ambapo alisisitiza kuwa, kazi iliyobaki ni kuinadi Ilani mpya ya CCM ya Uchaguzi Mwaka 2025 – 2030 kwa nguvu zote.
Mbeto alisema, hakuna Chama cha Siasa wala mgombea atakayehimili kimbunga cha Kampeni za CCM ambazo zitaanza Miezi michache ijayo toka sasa.
Alisema, Uwasilishaji wa taarifa ya matokeo ya Ilani Uchaguzi ya Mwaka 2020-2025, tija na mafanikio ya utekelezaji wa maendeleo ya kisekta, kumedhihirisha nia thabit walionayo Marais; Dkt. Samia Suluhu Hassan na mwenzake, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
“Wajumbe wa Mkutano Mkuu wameondoka Dodoma wakiwa wamebeba vikapu vya matumaini ya ushindi. Silaha ya ushindi wa chama cha siasa hutokana na ubora wa Ilani, sera na mipango ya maendeleo,” alisema Mbeto.
Aidha, Katibu huyo Mwenezi alisifu kazi kubwa iliyofanywa na Serikali zote mbili katika azma ya kutumikia wananchi na kuweka mkazo katika utatuzi wa changamoto za maendeleo ya kisekta.
Alisema, matokeo ya utekelezaji wa Ilani iliyopita ya Mwaka 2020-2025, imeelezea mafanikio ya Sekta za Afya, Elimu, Uwekezaji, Miundombinu, Nishati ya Umeme na gesi, Ufugaji na ukuzaji Kilimo.
”Taifa limepiga hatua nyingi za kimaendeleo hususan katika sekta ya Usafiri, Mawasiliano na Makaazi ya Nyumba bora za kisiasa, ujenzi wa Masoko, Barabara, Shule za Msingi na
Sekondari ikiwemo Ujenzi wa Vituo vya Afya na Zahanati,” alieleza.
Pia, alisema Ilani iliyopita imetaja na kuonyesha mafanikio katika ukuaji wa Uchumi wa Taifa, pato la Taifa, Viwanda, Uhusiano wa Kimataifa, Diplomasia, Michezo na Siasa pia mikopo ya taaisis za kimatiafa na Elimu ya juu.
Kadhalika Mbeto alisema, taarifa katika ilani iliyopita imeonyesha jinsi halmashauri za wilaya zilivyoanzisha miradi ya Maji Safi na Salama, Barabara za Vijijini, Wilaya na Mikoa hadi kukamilika kwake.
“Matumaini makubwa ya Wananchi yamebebwa na ilani mpya Uchaguzi wa Mwaka huu 2025-2530. Utekelezaji wa mipango iliyomo katika ilani hiyo itaipaisha na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi za uchumi Kati,” alieleza Katibu huyo Mwenezi.