Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
KATIBU wa Kamati Maalum NEC, Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis amesema, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) chini ya uongozi wa Dkt. Hussein Mwinyi imewekeza zaidi kwenye miundombinu ya Barabara ili kuchochea Uchumi.
Mbeto alisema hayo hivi karibuni muda mfupi kabla ya ufunguzi wa Barabara ya juu (flyover) ya Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Mwanakwerekwe, Mkoa wa Mjini Magharibi, ambapo alisisitiza ili uchumi upande, ni lazima uwekeze zaidi kwenye miundombinu.
Alisema, jambo hilo Zanzibar wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa, ambapo kila kona; Unguja na Pemba, wamejenga miundombinu mizuri hususani kwenye maeneo ambayo yana uzalishaji mkubwa wa mazao, hivyo imewasaidia wakulima kusafirisha mazao yao kwa urahisi.
Mbeto alisema, kwasasa wakulima hawana changamoto ya usafirishaji wa mazao yao na hawalazimiki kutumia magari yanayokokotwa na ng’ombe kulifikia soko, kwasababu wamefikiwa na miundombinu kwenye maeneo yao.
“Eneo lote la uzalishaji wa mazao, limepitiwa na miundombinu, hiyo maana yake ni kwamba unamfanya mkulima aone faida ya kilimo chake; anafikisha mazao yake kwa wakati na kwa muda,” alisema Mbeto.
Mbeto alisema yote hayo yanayofanyika ni mwendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) sambamba na kutimiza kwa vitendo kauli mbiu ya Dkt. Mwinyi ya ‘uongozi unaoacha alama.’
Kupitia kauli mbinu hiyo, Rais Dkt. Mwinyi amefanya jitihada kubwa za kuhakikisha mambo ya msingi yanayorahisisha shughuli za uchumi kwa wananchi, wanayafanyika kazi, ambapo mbali na miundombinu, anaboresha suala la elimu kwa ajili ya kuwawezesha vijana wote wa Zanzibar wawe na uelewa mpana.
“Lazima tuwatengeneze vijana wa Zanzibar wawe na uwezo hata kama haujamuajiri Serikalini, lakini anaweza yeye mwenyewe akatafuta utaratibu akajiajiri kwasababu amepata uelewa,” alisema Mbeto.