Mbeto amtaja Rais Dkt. Samia kiongozi shupavu Afrika Mashariki

0

Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema watu wanaojaribu kulifuja jina na uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hawatafikia malengo hayo kwasababu chini ya uongozi wake yapo mengi mazuri ya kutajika yamefanyika kwa maslahi ya Taifa.

Pia, CCM kimeutaka upinzani kuushukuru utawala wa Awamu ya Sita kutokana na juhudi za kufanikisha kupata maridhiano na kufungua ukurasa mpya.

Mbeto Khamis Mbeto, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo ameeleza hayo huku akiutaka upinzani kuacha Siasa za ushabiki, chuki na jazba.

Mbeto alisema, wakati Rais Dkt. Samia akiingia madarakani, aliikuta nchi ikiwa katika mkwamo wa demokrasia, kudorora kwa biashara, kutoaminiana na kupwaya kwa mahusiano mema na baadhi ya nchi jirani.

Si hivyo tu, alisema kulikuwa na malakamiko mengi kutoka kwa Wafanyabiashara wakubwa; wa kati na wadogo pia akiba za watu kupekuliwa kwenye Mabenki pamoja na baadhi ya Wanasiasa wa Chadema kukimbia nchi.

“Rais Dkt. Samia jina lake halitachafuliwa kwa hadithi za kutunga kwenye mitandao ya kijamii. Ni kiongozi shupavu, muungwana anayependa maridhiano. Ni kati ya viongozi wachache Afrika wenye utashi na uthubutu alionao,” alisema Mbeto.

Aidha, Katibu huyo Mwenezi alisema mara baada ya kuapa na kuwa Rais, Dkt. Samia alihakikisha anashughulikia kadhia zote zilizotishia mpasuko na mmomonyoko wa Umoja wa Kitaifa.

”Leo kuna baadhi ya wanasiasa wasio na kumbukumbu wameshasahau yaliowasibu akawafariji. Serikali yake imekamilisha Miradi mikubwa ya kimkakati na kuanzisha mengine pia imekamilika,” alieleza.

Hata hivyo, Mbeto alisema kutokana na juhudi za Serikali yake na hatua kubwa zilizofikiwa kimaendeleo, wapo waliodhani asingeifikisha nchi katika kilele cha maendeleo yaliyopo.

“Kwa uungwana na kujali utu ameanzisha kanuni ya Nne iliyoleta mapatano ya kijamii na kisiasa. Utawala wake umeruhusu mikutano ya hadhara. Dkt. Samia ni mpenda haki na Mwanademokrasia jasiri,” alifafanua Mbeto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here