Na Mwandishi Wetu, MAELEZO
RAIS wa Chama cha Mawakili wa Serikali nchini (PBA), Wakili Amedeus Shayo amesema Chama hicho kinatarajiwa kufanya mkutano mkuu wa Kitaifa wa mwaka utakaowakutanisha Mawakili Serikali Nchi nzima.
Mkutano huo unatarajiwa kufanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma kuanzia Aprili 14 hadi 15, 2025 ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt. Doto Mashaka Biteko.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Aprili 12, 2025 jijini Dodoma, Wakili Amedeus Shayo amesema mkutano huo pamoja na mambo mengine utakua jukwaa la kutathmini utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan alilolitoa Septemba 29, 2025 alipokuwa akizindua rasmi chama hicho ambapo aliwataka Mawakili hao wawe walinzi wa maslahi ya Taifa katika eneo la uchumi, mali za umma, mifumo ya kisheria ya uwekezaji na biashara.
Wakili Shayo ameeleza kuwa, kwa mujibu wa Ibara ya 59 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndiye mshauri Mkuu wa Serikali kuhusu masuala yote ya kisheria ambapo Mawakili wa Serikali hutekeleza majukumu yao kwa niaba yake akiongeza kuwa Mawakili hao wanabeba jukumu la kikatiba la kulinda maslahi ya Taifa Kwa njia ya Sheria.
“Lengo kuu la kuanzisha Kwa Chama cha Mawakili wa Serikali ni kuwa jukwaa la kitaaluma ambalo linawaleta pamoja Mawakili wa Serikali katika kujadili maslahi ya pamoja ya Mawakili wa Serikali, kusimamia maendeleo ya Sekta ya Sheria, kushughulikia maadili, miiko na maendeleo ya tasnia ya Sheria ndani ya Utumishi wa Umma, kukuza ubora na weledi katika fani ya sheria kupitia mafunzo ya kujenga uwezo” alisema Wakili Shayo.
Alisema, mkutano wa mwaka huu utawahusisha Mawakili na Maafisa Sheria wote wanaotoa huduma za kisheria katika Utumishi wa Umma kwenye Wizara, Idara, Taasisi, Mamlaka, mashirika na Wakala, Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa ambao wamesajiliwa katika daftari la Mawakili wa Serikali ambalo linasimamiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Katika hatua nyingine Wakili Shayo ametoa Rai kwa waajiri wote wa Umma zikiwemo Wizara, Idara, Wakala, Mashirika ya Umma, Taasisi na Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ziwaruhusu Mawakili na Maafisa Sheria wa Serikali walio chini kushiriki Mkutano huo Mkuu wa Kitaifa.