Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Jenista Mhagama ameelekeza watendaji wa Idara ya Menejimenti ya Maafa katika ofisi hiyo kuhakikisha wanaweka utaratibu wa kimfumo ili misaada yote iingie kwenye mfumo rasmi ili iweze kuwafikia wale waliokusudiwa.
Ametoa kauli hiyo wakati akipokea vifaa vya msaada wa kibinadamu vilivyowasilishwa na wadau mbalimbali kusaidia wahanga wa maafa yaliyotokana na maporomoko ya mawe na tope kutoka mlima Hanang Mkoani Manyara.
Waziri Mhagama alisema, Serikali imepokea misaada hiyo huku akishukuru kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuwahakikisha kuwa misaada hiyo itasimamiwa kwa ukaribu ili kuhakikisha inaleta tija kwa wahusika.
“Kipekee niwapongeze na kuwashukuru sana kwa namna mlivyoguswa na kuungana na Serikali katika kuwanusuru ndugu zetu waliopatwa na maafa haya, Hanang Tunawashukuru sana,” alisisitiza.
Alitumia nafasi hiyo kutoa onyo kwa yeyote atayejaribu kufanya utapeli au kujinufaisha isivyo halali katika kipindi hiki.
“Tumewaonya matapeli wasije wakathubutu kutengeneza akaunti za utapeli kwa sababu tutawakamata na Serikali itachukua hatua kali za kisheria,” alibainisha
Waziri Mhagama alitumia nafasi hiyo kueleza umma kuwa Serikali imetoa akaunti sahihi ya kutuma michango ya kifedha kwa ajili ya masuala ya maafa ambapo ni kwa akaunti ya bank yoyote ya ndani au nje ya nchi.
“Kwa ajili ya kukabiliana na maafa ya Katesh itatumika Akaunti ya Mfuko wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa (National Disaster Management Fund Electronic Account) Na. 9921151001 kwa kuandika neno maafa likifuatiwa jina la Wilaya ya Hanang’.
Halikadhalika alitoa rai kwa watumishi watakaohusika na misaada itakayotolewa kuhakikisha wanafanya kazi kwa uaminifu ili misaada iwafikie walengwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Kupitia Chama Cha Mapinduzi Mary Chatanda alisema anatoa pole kwa niaba ya Umoja wa wanawake Tanzania kwa tukio hilo lenye kuleta majonzi na huzuni kubwa kwa wana Hanang’, jamii na Taifa kwa ujumla.
Tunashukuru wafadhili mbalimbali wameweza kutuchangia, tumekuja na Mablanketi 120, mashuka 300, mashuka ya kimasai 500, madira ya kuvaa wanawake 520, kanga 1000, katoni za sabuni na mafuta ya kupaka,” alisema.
Aidha, alitoa rai kwa jamii, wadau mbalimbali kuendelea kujitokeza kusaidia ili kuwapa nafuu waliofikwa na maafa hayo. “Wabunge wetu wa viti maalum nao wamesaidia kuchangia kupitia kwa Katibu wao wa wabunge na fedha hizo tutawasilisha baadae.”