MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema maendeleo yanayoonekana hivi sasa katika sekta mbalimbali Zanzibar ikiwemo sekta ya elimu ndiyo lilikuwa lengo la Mapinduzi Matukufu ambayo yalidhamiria kuboresha Maisha ya watu.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa Ufunguzi wa Skuli ya Sekondari ya Makunduchi iliyopo Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Amesema hivi sasa inashuhudiwa ndoto ya waasisi wa Mapinduzi Matukufu ikiendelea kutimizwa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Makamu wa Rais amesema fursa za masomo kwa wananchi wa Zanzibar zimeongeza ambapo, wakati wa Mapinduzi mwaka 1964, kulikua na Skuli 68 hivi sasa kuna zaidi ya skuli 1200, waliokuwa masomoni mwaka 1964 walikua elfu ishirini na tano hivi sasa zaidi ya wanafunzi laki sita wanapata elimu pamoja na kuwa na Vyuo Vikuu Vitano hivi sasa ikilinganishwa na mwaka 1964 ambapo hakukuwa na Chuo Kikuu.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema, Serikali imeendelea kufanya mabadiliko makubwa ya Mitaala ambayo imejielekeza katika kufundisha kujimudu katika kufikiri kutafiti na kubuni pamoja na mafunzo kwa vitendo.
Ameongeza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweza kuimarisha mitaala yake na kujielekeza katika ufundishaji wa kiteknolojia na kuboresha miundombinu ya maabara na madarasa na mfumo utakaowezesha vijana kujitegemea kupitia uwepo wa mkondo wa masomo ya jumla na masomo ya amali.
Makamu wa Rais ametoa wito kwa wananchi wote kuendelea kuenzi na kulinda amani kwa namna yeyote kwa kuwa maendeleo yeyote yanahitaji uwepo wa amani na utulivu.
Amesema katika kipindi cha miaka 62 tangu Mapinduzi Matukufu, matunda ya Muungano yameonekana wazi ambapo, Tanzania imeendelea kuulinda na kuutetea uhuru, umoja, maendeleo, pamoja na amani.
Makamu wa Rais amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa maendeleo makubwa katika kipindi cha miaka mitano pamoja na kulinda Muungano na Amani.
Vilevile, Makamu wa Rais amewapongeza wananchi waliojitolea kwa uzalendo sehemu ya ardhi kwaajili ya kufanikisha ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya Makunduchi.