Na Mwandishi Wetu
MABORESHO yaliyofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Uchukuzi katika bandari nchini yameongeza wingi wa shehena kupitia bandari mbalimbali ambazo zimechangia ukuaji wa uchumi maradufu nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa katika bandari ya Dar es Salaam, msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa akielezea mafanikio ya siku mia moja za Uongozi wa Raisi Samia Suluhu Hassan tangu alipoingia madarakani Novemba 3, mwaka jana.
“Maboresho hayo yamewezesha bandari za Tanzania katika mwaka wa 2024/2025 kuhudumia shehena za zaidi ya tani milioni 12 ambazo zimeenda katika nchi zinazotuzunguka za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia, Burundi, Rwanda, Uganda, Zimbabwe, Malawi na nyinginezo”, alisema Msigwa.
Alisema, kwa shehena hizo nchi imeingiza kiasi cha shilingi trilioni 12.33 katika kipindi cha mwaka 2024/2025, ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 17 ikilinganishwa na makusanyo ya shilingi trilioni 10.55 kwa mwaka 2023/2024.
Msigwa alisema, kati ya kiasi hicho cha shehena, nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inaongoza kwa kupokea shehena nyingi zaidi kutoka kwenye bandari za hapa nchini, ambapo wamepitisha zaidi ya tani milioni tano, kwa kipindi cha mwaka 2024/2025 na hiyo yote ni kutokana na maboresho ya miundombinu mbalimbali katika bandari za maziwa na bahari.
Pamoja na hayo, Msigwa alisema mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ilisaini mkataba na DP World na Tanzania East Africa Gateway Terminal (TEAGTL) kwa ajili ya kusimamia uendeshaji wa bandari ya Dar es Salaam pamoja na kuboresha miundombinu mbalimbali bandarini hapo.
“Kampuni hizi mbili kwa pamoja zimewekeza zaidi ya bilioni 624 kwa ajili ya maboresho mbalimbali ambayo baadhi ya hayo yamekamilika na mengine yanaendelea kurekebishwa”, alibainisha Msigwa.
Alisema, maboresho yaliyofanywa na kampuni hizo mbili ni pamoja na mitambo mipya ya kushushia na kupakia makasha, ambapo hivi sasa ni ya kisasa na inafanya kazi hiyo kwa haraka zaidi, usanifu na uboreshaji wa mifumo ya tehama, pamoja na ukarabati wa karakana ya mitambo.
Msemaji huyo aliendelea kuelezea maboresho mengine yaliyofanywa na kampuni hizo ni pamoja na kuendeleza maeneo mbalimbali ya kuhifadhia shehena ili kuiongezea uwezo bandari ya Dar es Salaam hasa pale ambapo shehena zinakuwa nyingi.
“Maboresho hayo yamezaa matunda lukuki ambayo ni pamoja na ongezeko la shehena hadi kufikia tani milioni 27.7 katika mwaka wa fedha 2024/2025 ikilinganishwa na tani milioni 23.69 kwa mwaka 2023/2024 wakati wawekezaji hawa wanaanza kazi”, alibainisha Msigwa.
Msigwa aliongeza kuwa muda wa meli kuhudumiwa bandarini umepungua kutoka wastani wa siku 30 hadi kufikia wastani wa siku 6 kwa meli za makasha, na hii inajumuisha muda wa kusubiri nangani, na hiyo yote ni kutokana na uwepo wa vifaa vya kisasa vya kushushia makasha.
Pamoja na hayo, Msigwa alisema uwekezaji huo umewagusa wananchi wa kawaida moja kwa moja kwa kupata ajira kwenye makampuni ya DP World pamoja na TEAGTL katika fani mbalimbali kama vile makarani wa shughuli za uendeshaji, waendesha mitambo mikubwa na midogo.
“Watanzania zaidi ya 764 wamepata ajira za moja kwa moja na wengine wamepata ajira zisizo za moja kwa moja, ajira hizo hujumuisha wafanyakazi wa kutwa, madereva wa malori, na mawakala wa forodha,” alifafanua.
Licha ya haypo TPA inaendelea na maboresho ya kimkakati ya miradi mbalimbali kama vile ujenzi wa gati na matenki ya kuhifadhia mafuta ambapo mpaka sasa ujenzi waje umefikia asilimia 35, na ujenzi wa gati namba 8 hadi 11 na ujeni wa gati namba 12 mpaka 15.
Kwa upande wa bandari ya Dar es Salaam wanaendelea na ujenzi wa reli za MGR, SGR na TAZARA, mradi huu ukikamilika utaongeza ufanisi wa kuhudumia shehena ya makasha hadi 480,000 kwa mwaka na kuwezesha usafirishaji wa shehena kwa njia ya reli kuongezeka kutoka asilimia 2 ya sasa hadi asilimia 12.