Makonda amtaka Mbowe kuacha upotoshaji

0
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda.

Na Mwandishi Wetu

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda ‘amemvaa’ Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akimtaka aache kuendeleza tabia ya upotoshaji kama kete yake kubwa ya kufanya siasa nchini.

Makonda alisema hayo alipozungumza na vyombo vya habari mjini Zanzibar, kuhusu hoja mbalimbali dhidi ya upotoshaji uliofanywa na Chadema, kupitia kwa Mwenyekiti wao hivi karibuni.

Alisema, chini ya Uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Watanzania wameshuhudia haki ikisimamiwa kikamilifu.

Makonda alisema, miongoni mwa mambo aliyoyafanya Rais Samia ni kuunda Tume ya Haki Jinai na kupitia mambo kadhaa ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata haki yake bila kujali rika, elimu kipato, kabila, dini na hata kule alipotokea.

“Kwa masikitiko makubwa tumepata nafasi ya kumsikia kaka yetu Freeman Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa CHADEMA akituhumu na kutoa kauli za kuzalilisha na kufedhehesha na kutweza utu wa Kiongozi wetu bila kujali dhamira njema aliyoonyesha Mwenyekiti wetu wa CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ujenzi wa Umoja na Mshikamano katika Taifa letu,” alisema.

Aliongeza: “Mbowe kasema maneno mazito sana, upo wakati tumetafakari ya kwamba hakuna sababu ya kumjibu lakini imefika wakati tukasema Hapana…kwanini tumuache apotoshe umma kwa kitu ambacho hatuelewi msingi wake ni nini?”

Makonda alisema, Mbowe anafahamu katika mapendekezo 84 yaliyotolewa, mapendekezo 63 yote yamechukuliwa na yapo kwenye muswada ambao hatua za kisheria zinaendelea katika kuunda kwa sheria na yeye ni mnufaika mkubwa wa maridhiano ambayo yamemfanya akawa huru na kesi zote za kisiasa bila masharti yoyote.

“Mbowe yeye mwenyewe na chama chake na vingine vimeruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara bila kubughudhiwa tena kwa ulinzi mkali chini ya Jeshi la Polisi kuhakikisha dhamira ya Rais Samia inatimia si tu kwa vyama vya siasa bali kwa Watanzania wote,” alisema Makonda.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here