Na Joseph Zablon, Dar es Salaam
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kinakabiliwa na mgogoro ndani ya chama na sasa wanatumia ‘No reform No Election’ kama kichaka cha kujificha kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.
Akizungumza wakati wa mkutano na viongozi wa ngazi ya mitaa wa Jimbo la Ubungo, Jijini Dar es Salaam leo, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makalla alisema, ndani ya Chadema kuna ‘Bundi’ na siku si nyingi kila kitu kitakuwa bayana.
“Kuna watu wanataka wagombee nafasi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Ubunge, Udiwani na Viti Maalum ambao hawakubaliani na hicho anachokinadi Mwenyekiti wao, Tundu Lissu” alisema Makalla na kuwashangaa ni mabadiliko gani wanayoyataka.
Alisema, mabadiliko ya Katiba yaliyofanyika mwaka jana ikiwa ni katika yale ambayo upinzani walikuwa wanayalalamikia, cha ajabu yamefanyika lakini bado wanasema ‘No Reform No Election’ (hakuna marekebisho, hakuna uchaguzi).
Alisema, hawana nia njema kwani awali walisema uchaguzi unasimamiwa na wakurugenzi wa halmashauri, kipengele hicho kimeondolewa sasa wasimamizi wa uchaguzi wataomba na majina yao kuchujwa na jopo litakalokuwa na Jaji Mkuu wa Bara na Zanzibar.
“Kimewekwa kipengele cha hakuna kupita bila kupingwa walichokuwa wakitaka na suala la pingamizi litawekwa na mpiga kura au mgombea sasa sijui wao wanataka nini..?”
Alisema, hata wanapotaka katiba mpya ni mchakato ambao hauwezi kushughulikiwa kwa siku mbili kama wanavyotaka wao kwani lazima uhusishe wadau mbalimbali.
“Hata wanaposema nguvu ya umma sijui ni umma upi maana kama wanachama CCM inao wengi kuliko chama kingine chochote,” alisema na kuongeza kuwa wanachama wa chama hicho wajipange kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu 2025.
Upande mwingine, Makalla aliwaonya wanaCCM wanaojipitisha hivi sasa kabla wakati haujafika kuwa wanakisaidia chama kukata majina yao wakati ukifika.
“Kuna watu wanapita pita huko kwenu wajumbe, wengine wanajifanya kusema mbona mbunge haonekani na kuna ambao wanajifanya wanasikiliza kero za wananchi,”
Alisema, wakati ukifika utatangazwa na wagombea watajitangaza na kuchukua fomu kuwania kupendekezwa na chama hicho kuwania nafasi za ubunge au udiwani lakini sio sasa.
Makalla alisema, CCM ni chama kikubwa na baada ya kumalizika kura za maoni ni lazima kuvunja makundi na kushikamana kukijenga chama na kuwatumikia wananchi.
Makalla alisema, wamebadili utaratibu wa kumpata mgombea kwa kuwataka wenye nia kuanzia kwenye mashina ili kujenga demokrasia zaidi na amewataka kujiandaa kwa ajili ya daftari la kudumu la wapiga kura.
“Zoezi la kujiandikisha na kurekebisha taarifa zenu kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kwa Dar es Salaam linaanza Machi 17 hadi 23 mwaka huu 2025, hivyo jitokezeni kwa wingi,” alisema Makalla.