Majaliwa: Serikali imejipanga kudhibiti magugumaji Ziwa Victoria

0

▪️Amshukuru Rais Dkt. Samia ununuzi wa mitambo ya uteketezaji wa magugumaji
 

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha changamoto ya uwepo wa magugumaji katika ziwa Victoria inapatiwa ufumbuzi ili kuwezesha shughuli za kijamii ziweze kuendelea katika maeneo hayo.
 
”Ninamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa fedha za ununuzi wa mitambo mikubwa ya kuteketeza magugumaji ndani ya ziwa Victoria ili kuwezesha shughuli za uvuvi, usafiri na usafirishaji kuendelea.”
 
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Mei 19, 2025) wakati akizungumza na wananchi alipokagua shughuli ya udhibiti wa magugumaji katika eneo la Kigongo-Busisi akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.
 
Majaliwa alisema, magugumaji hayo yamekuwa yakiathiri kwa kiwango kikubwa shughuli mbalimbali za kijami na kiuchumi katika ziwa hilo, hivyo ununuzi wa mitambo hiyo utasaidia kuteketezwa kwa magugu hayo.
 
Aidha, Waziri Mkuu amewashukuru wananchi wa maeneo hayo wakiwemo wavuvi ambao wamejitolea kushirikiana na Serikali katika zoezi la kuyaondoa magugumaji hayo.
 
Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameiagiza Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira iendelee na kazi ya kuyaondoa magugumaji hayo hadi pale yatakapomalizika ili kuhakikisha shughuli za kijami zinaendelea bila ya kikwazo chochote.
 
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhandisi Cyprian Luhemeja akitoa taarifa kuhusu shughuli ya kuteketeza magugumaji hayo kwa Waziri Mkuu amesema kwa sasa wanaendelea na kazi ya kuyaondoa magugumaji ya asili ambayo yamesambaa katika eneo la ukubwa wa ekari zaidi ya 300.
 
Alisema, magugumaji hayo ambayo yamegawanyika katika aina tatu (salivinia molesta ambalo ni jipya, water hyacinth na gugumaji la asili aina ya Lutende) yameathiri mfumo wa ikolojia, shughuli za usafiri na usafirishaji na shughuli za uvuvi katika baadhi ya maeneo ndani ya Ziwa Victoria
 
Katibu Mkuu huyo alisema, wanatarajia kumaliza kazi ya kuyateketeza magugumaji mwezi Julai, 2025 na hivyo kuwezesha shughuli za uvuvi, usafiri na usafirishaji kuendelea katika ziwa Victoria kama ilivyokuwa awali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here