SPINEL ni miongoni mwa madini ya vito yenye thamani kubwa sana duniani, yanayoendelea kupata umaarufu mkubwa katika masoko ya Kimataifa kutokana na ubora wake wa kipekee, rangi adimu na uimara wa hali ya juu.
Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zilizojaaliwa rasilimali hii adimu, hususan katika eneo la Mahenge, Kijiji cha Epanko, Wilaya ya Ulanga, mkoani Morogoro, eneo ambalo limejijengea sifa ya kuwa chanzo cha spinel bora zaidi duniani.
Spinel ni jiwe la vito lenye rangi mbalimbali ikiwemo nyekundu, pinki, zambarau, bluu na machungwa. Umaarufu wake unatokana na sifa kadhaa muhimu ikiwemo uwazi wake wa hali ya juu (high clarity), rangi kali na ya kuvutia inayopendwa sana katika soko la vito, pamoja na uimara mkubwa unaoufanya kudumu kwa muda mrefu.
Aidha, spinel nyingi hupatikana bila kuhitaji matibabu ya joto (heat treatment), jambo linaloongeza thamani yake sokoni.
Kwa miaka mingi, spinel nyekundu ilichanganywa na ruby hadi pale sayansi ya madini ilipobaini tofauti zake. Leo hii, spinel imesimama kama jiwe la vito lenye hadhi yake binafsi na thamani inayozidi kuongezeka mwaka hadi mwaka.
Mahenge, iliyopo Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro, ni eneo lenye umuhimu mkubwa katika ramani ya madini ya vito duniani. Spinel inayopatikana Mahenge inajulikana kwa rangi yake ya pinki na nyekundu yenye mwanga wa kipekee (neon-like glow), sifa inayofanya spinel ya Mahenge kutafutwa sana na wafanyabiashara wa vito duniani.
Ugunduzi wa spinel katika eneo hili umeifanya Mahenge kutambulika kimataifa na kuiweka Tanzania miongoni mwa nchi muhimu katika biashara ya madini ya vito. Spinel ya Mahenge imekuwa ikitajwa mara kwa mara katika maonesho makubwa ya vito ya kimataifa ikiwemo Tucson Gem Show nchini Marekani, Hong Kong Jewellery Fair, pamoja na maonesho ya vito ya Bangkok, Thailand, hatua inayoongeza hadhi ya Tanzania katika soko la kimataifa la madini ya vito.
Uchimbaji wa spinel Mahenge unaongozwa na kampuni za Kitanzania, zikiwemo Ruby International Limited na Franone Mining, ambazo ndizo wawekezaji wakuu katika uchimbaji wa madini haya katika eneo hilo. Kampuni hizi, ambazo ni mali ya Watanzania, zimeonesha mfano mzuri wa jinsi wawekezaji wa ndani wanavyoweza kuendeleza rasilimali za taifa kwa ufanisi, uwajibikaji na uzingatiaji wa Sheria.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa spinel ya Mahenge na mchango wake kwa jamii, Msimamizi wa Ruby International Mining, Mhandisi Penina Mtego, katika mgodi wa Epanko, Mahenge, anasema:
“Spinel ya Mahenge ni rasilimali adimu yenye ubora wa kipekee duniani. Kama kampuni ya Kitanzania, tumedhamiria kuhakikisha uchimbaji wake unazingatia viwango vya kitaalamu huku manufaa yake yakirudi moja kwa moja kwa taifa na kwa wananchi wa Mahenge. Kipaumbele chetu ni kutoa ajira, kuchangia maendeleo ya jamii na kulinda mazingira.”
Msimamo wa Serikali
Serikali ya Tanzania inaendelea kusisitiza umuhimu wa kusimamia rasilimali za madini kwa tija na uwazi ili ziwe chachu ya maendeleo ya wananchi. Akizungumzia mchango wa madini ya vito, hususan spinel ya Mahenge, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, anasema:
“Madini ya vito kama spinel ya Mahenge ni utajiri mkubwa wa taifa letu. Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wazawa ili kuhakikisha rasilimali hizi zinachimbwa kwa kuzingatia Sheria, zinawanufaisha wananchi, na kuongeza mapato ya serikali kwa maendeleo ya nchi.”
Kauli hiyo inaakisi dhamira ya serikali ya kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika sekta ya madini na kuongeza thamani ya rasilimali kabla ya kuingia kwenye masoko ya kimataifa.
Uwepo wa migodi ya spinel Mahenge unaleta mabadiliko makubwa ya kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa eneo hilo. Vijana wengi pamoja na kina mama wamepata ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja katika shughuli za uchimbaji, ulinzi, usafirishaji na huduma mbalimbali.
Dkt. Kiruswa anasisitiza kuwa, ajira hizi zimekuwa chanzo muhimu cha kipato kwa familia nyingi, hivyo kusaidia kupunguza umaskini na kuboresha hali ya maisha ya wakazi wa Mahenge na maeneo ya jirani.
Mbali na kutoa ajira, Dkt. Kiruswa anazipongeza Kampuni za Ruby International Limited na Franone Mining kuwa kuendelea kutekeleza wajibu wao kwa kijamii kwa kuchangia maendeleo ya jamii inayozunguka migodi yao ambapo mchango huo unajumuisha: Ujenzi wa zahanati, ujenzi na ukarabati wa shule na madarasa, ujenzi wa ofisi za serikali za mitaa, kuboresha miundombinu ya barabara, kuchangia ustawi wa vijana na wanawake na ushirikiana kwa karibu na viongozi wa eneo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Mahenge.
Hatua hizi zinaonesha dhamira ya dhati ya kampuni hizi katika kuhakikisha rasilimali za madini zinaleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.
Utalii wa Madini na Fursa Mpya za Kiuchumi
Uwepo wa madini ya spinel Mahenge umechochea pia kukua kwa utalii wa madini, ambapo wadau wa ndani na nje ya nchi wanafika Mahenge kujifunza, kuona na kushuhudia shughuli za uchimbaji wa madini ya vito.
Utalii wa madini Mahenge umeanza kuchangia kukua kwa uchumi wa eneo hilo kwa kuleta fursa mpya katika sekta za malazi, usafiri, uuzaji wa vito pamoja na kukuza utamaduni wa wenyeji.
Spinel ni hazina kubwa ya taifa ambayo imeipa Tanzania heshima na nafasi ya kipekee katika soko la madini ya vito duniani. Mahenge, Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro, imekuwa mfano bora wa namna rasilimali asili zinavyoweza kuleta maendeleo endapo zitasimamiwa kwa uwazi, uzalendo na uwajibikaji.
Kupitia uwekezaji wa kampuni za Kitanzania kama Ruby International Limited na Franone Mining, spinel imekuwa chanzo cha ajira, mapato na maendeleo ya kijamii, kuthibitisha kuwa uwekezaji wa wazawa katika rasilimali za taifa ni nguzo muhimu ya maendeleo endelevu ya nchi.
Kutokana na ubora wa madini hayo, rasilimali hii bado inahitaji uwekezaji wa kutafiti, kuchimba, biashara na kuongezwa thamani fursa hizi bado zipo na ikizingatiwa kwa mujibu wa wataalam kwa vito ni aina 25 tu vinazochimbwa Tanzania huku kukiwa na zaidi ya aina 100 za madini ya vito ambayo nchi hii imebarikiwa kuwa nazo. Kwa wageni Sheria inaruhusu kuingia mkataba wa usaidizi kupitia teknolojia na mitaji.