Magonjwa ya akili yanaweza kumpata mtu yeyote

0

Na Dkt. Raymond Mgeni

HOSPITALI zote hapa nchini zimekuwa na jitihada kubwa za kutoa huduma za matibabu dhidi ya magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa sugu yasiyoambukiza kama magonjwa ya moyo, kisukari na kundi la magonjwa yakuambukiza, huduma za kulaza, kliniki, huduma za vipimo na uchunguzi.

Pamoja na jitihada hizo za kumsaidia mwananchi kila mmoja kadiri ya tatizo lake, bado kumekuwa na utofauti mkubwa wa utoaji huduma za afya ya akili katika hospitali za binafsi mbalimbali hapa nchini.

Hii ni kutokana na mtazamo kwamba, magonjwa ya akili ni kwa watu wenye kipato duni na hawawezi kumudu gharama za matibabu katika hospitali za binafsi, jambo ambalo si kweli, kwani magonjwa ya akili humpata mtu yoyote haijalishi kipato chake, elimu yake au wadhifa alionao.

Ukweli ni kwamba, wenye kipato kikubwa ni wepesi wa kutafuta huduma za afya ikiwemo huduma za akili kwa gharama yoyote ile hata kama zipo kwa huduma za hospitali za binafsi.

Hospitali za binafsi na asasi za dini zinazotoa huduma za matibabu zimekuwa zikikwepa kutoa huduma hizo za afya ya akili kwa wateja wake hata kama wanatumia bima za afya; wagonjwa hao wa akili huambiwa waende katika hospitali za Serikali za rufaa kwa ajili ya huduma hiyo na hata katika mabango ya hospitali za binafsi huwa hakuna tangazo kwamba wanatoa huduma za afya ya akili.

Msisitizo wa malengo mkakati ya maendeleo ya Dunia ya mwaka 2030 ni kukabiliana na kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya na matibabu stahiki ya magonjwa ya akili. Hili ni dhahiri kwamba suala hili bado halitekelezwi kwani hata kwa hospitali za serikali.

Hospitali nyingi ya wilaya hazitoi huduma za matibabu ya afya ya akili kama kwa wagonjwa wengine wa nje na wagonjwa wa ndani.

Hospitali nyingi za wilaya zinatoa matibabu ya kliniki kwa wagonjwa wa akili na hazina wodi za kulaza wagonjwa wa akili pale inapohitajika mgonjwa huyo alazwe na hivyo mgonjwa huambiwa aende kupatiwa matibabu hospitali ya rufaa angali hana uwezo wa kumudu gharama za matibabu ngazi ya rufaa ikiwa ni pamoja na ndugu kwenda kumuona mgonjwa wao akiwa amelazwa huko.

Kukosekana huko kwa huduma za kulazwa kwa mgonjwa wa akili, ndugu huamua kurejea nyumbani na mgonjwa wao bila kupatiwa matibabu na kumfungia ndani ili asiwasumbue na kuleta uharibifu.

Suala hili la hospitali za wilaya si kwa hospitali za Serikali tu, bali hata kwa hospitali teule za wilaya ambazo zina milikiwa na taasisi za dini ama mtu binafsi; nazo hazitoi huduma za afya ya akili kwa wagonjwa wa akili hususani wagonjwa wanaohitaji kulazwa angali inalaza magonjwa mengine yote.

Hospitali za binafsi na taasisi za dini zikumbuke kuwa, kila mtu ni mgonjwa isipokuwa hajaweza kufikia vigezo vya kuwa mgonjwa wa akili, hivyo wanapotoa huduma za magonjwa sugu mfano kisukari, magonjwa ya moyo, huduma za mama na mtoto wagonjwa hao hao wanao wahudumia ni rahisi kupatiwa matibabu.

Pia, ni rahisi kupatwa na matatizo ya kisaikolojia na kupatwa na ugonjwa wa akili na hivyo mgonjwa huyo ana haki ya kupatiwa huduma mjumuisho ili kuweza kuimarisha afya yake kwa ujumla.

Mfano, hospitali zote zinazotoa huduma ya mama na mtoto ni muhimu kutoa huduma za afya ya akili na kisaikolojia kwani wajawazito wengi na akina mama wanaonyonyesha hukumbana na changamoto mbalimbali katika maisha yao.

Miongoni mwa changamoto hizo ni kutelekezewa watoto na wenza wao, sonona itokanayo na kubadilika kwa mfumo wa maisha aliyoyazoea, kushindwa kupokea ipasavyo ujio wa mtoto, kulaumiwa na wenza wao kutokana na kupata watoto wa jinsia moja kila mara, kuzaa mtoto mlemavu na mengineyo mengi.

Mambo hayo yote humsababisha mama mjamzito ama mama anayenyonyesha kushindwa kumlea mtoto ipasavyo na anapofika katika kituo binafsi cha huduma za afya kukosa huduma za kisaikolojia na matibabu ya afya ya akili isipokuwa hupatiwa huduma za kliniki za kawaida za ujauzito angali ana msongo wa mawazo (sonona).

Aidha, inapofikia hatua ya mgonjwa kuchanganyikiwa anapofikishwa katika hospitali ya Serikali inayotoa huduma za afya ya akili, hali yake huwa mbaya na kumuongezea mgonjwa au ndugu gharama kubwa za matibabu.

Kutokana na hali hiyo, upo umuhimu mkubwa wa hospitali za binafsi na taasisi za dini kuanza kutoa huduma za afya ya akili kwa wagonjwa kwani magonjwa ya akili huambatana na uwepo wa magonjwa mengine na pia itakuwa ni silaha mojawapo ya kupambana na unyanyapaa kwa wagonjwa wa akili hapa nchini.

*Mwandishi wa makala hii ni mtaalamu kutoka Hospitali ya Kanda Rufaa Mbeya, Idara ya Afya ya Akili na Magonjwa ya Akili. Anapatikana kwa namba 0676 559 211. Barua pepe:- raymondpoet@yahoo.com.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here