Na Yusuph Katimba
NAKUMBUKA kwenye kikao kimoja cha ujenzi wa Chama cha ACT Wazalendo, muda mfupi baada ya Maalim Seif Sharif Hamad kuhamia, alishughulikiwa.
Yalikuwa maneno makali kutoka kwa mwanachama wa chama hicho Fatma Omar, aliyetokea Chama cha Wananchi (CUF). Kikao hicho kilifanyika Chokocho, Mkoa wa Kusini, Pemba.
Awali, Fatma alikuwa mwanachama wa CUF, baada ya Maalim Seif kufanyiwa vituko vya ukewenza ndani ya chama hicho, alihamia ACT Wazalendo. Fatma naye alihama kama walivyohamia wanachama wengine wa CUF.
Kwenye kikao hicho, Fatma alimvaa Maalim Seif kutokana na kile alichokiita upole usio na maana, alikwenda mbali zaidi na kumtuhumu kuchelewesha ‘haki’ yao kama Wazanzibari.
Fatma alionesha kwamba, Maalim Seif ndio kikwazo. Hakutamani njia aliyoitumia kutafuta haki akiamini njia hiyo, imepitwa na wakati – inawachelewesha.
Mwanamama yule alimshambulia Maalim Seif kwa kupoza ari ya wanachama walio na haraka na mageuzi. Alimwambiwa kwamba, anaendekeza Uislam badala ya kuwapeleka Wazanzibari kwenye lengo pasi na kujali njia watayopita.
Fatma ndani ya moyo wake, hakutamani kile kinachoitwa subra, alitaka kushuhudia Zanzibar ikiingia katika zama mpya za kiutawala. Kwa Fatma, kesho yake haikuwa na thamani isipokuwa leo.
Fikra ya Fatma ilijengwa na mapambano katika kupata haki. Hakuamini falsafa ya Maalim Seif kwamba, ipo siku kile anachokitaka kinaweza kupatikana bila vurugu, kumwaga damu ama kuchoma vituo vya mafuta. Fatma damu yake ilikuwa ikitokota huku ndita ikitawala paji lake la uso.
Kwenye kikao hicho, Fatma alijilipua kweli kweli kwamba, akimtazama Maalim Seif kwa jicho kavu, Fatuma alisema kila wakati wanachama wakiunga mkono harakati za ‘mabavu,’ Maalim Seif alikuwa akiwapa mgongo, akipinga kwa maneno laini.
“Kila tukikuunga mkono, tunaona wewe mwenzetu Uislamu umekujaa. Kwa hiyo mwenzetu, ikiwa Uislamu umekujaa, nafasi achia wenzio. Ukae nyuma, uwe mshauri kama ulivyo mshauri.
“Kwa sababu wewe kila tukija juu, (unatuambia) ‘tulieni, tulieni, tulieni.’ Hatutaki tena…, ikiwa nafasi imekushinda, (mwaka) 2020 ukae benchi, uwe mshauri,” ni maneno yaliyobeba ujasiri mzito kutoka kwenye sakafu ya moyo wa Fatma.
Katika kipindi chote hicho, Maalim Seif alikuwa kimya, akimtazama Fatma machoni. Viongozi wengine wa ACT Wazalendo hawakuthubutu kumfunga mdomo.
Maalim Seif aliendelea kuvumilia maneno makali kutoka kwenye kinywa cha Fatma aliyeonekana kuwa tayari kwa lolote, akisubiri ulimi wake utie nanga. Ukumbi ulikuwa kimya. Kama si sauti ya Fatma, basi hata sindano ingedondoka kila aliyekuwa pale angeisikia.
Alichokizungumza Fatma kilionekana kutoka moyoni kwake, alikuwa amekasirika kweli kweli. Hatimaye maneno yakamuisha, ulimi wake ukagota.
Baada ya Fatma kuweka nukta, hadhira yote ikageuza macho kwa Maalim Seif, ikisubiri nini kitatoka kwenye kinywa chake.
Maalim Seif hakuwa na haraka, alivuta sekunde kadhaa akitafakari namna ya kumrudi Fatma, aliamini wapo wengine wengi wenye mtazamo wa Fatma na aliamini si jibu la Fatma pekee bali na wale wenye mtazamo kama wake.
Baada ya dakika kadha za mashambulizi kutoka kwa Fatma Maalim Seif alisema:-
“Vurugu haina macho, au siyo?… ilikuwa kauli ya kwanza kutoka kwenye kinywa chake, alitoa sekunde kadhaa kana kwamba anasubiri jibu, na kweli jibu alilipata maana hadhira iliitikiwa kwa kutikisa kichwa ‘naam.’
Kwa sauti hafifu Maalim Seif aliendele “… (ikianza) hujui nani ataumia…. Vurugu si nzuri kwani haichagui nani ikamdhuru,” alisema Maalim.
Wakati Maalim Seif akitamka maneno hayo, alikuwa akimtazama Fatma usoni, naye Fatma hakuangalia pembeni. Mboni ya jicho lake ilikutana moja kwa moja na ile ya Maalim Seif. Fatma alikuwa ‘mkavu’ kweli kweli.
Hadhira iliendelea kuwa kimya ikisubiri hitimisho, huku kila mmoja akiwa na lake kichwani. Kabla ya kuhitimisha, Maalim Seif alikumbuka kauli ya mwanzo ya Fatma kwamba ‘Uislam umekujaa.’
“Tena na mimi nakiri (kwamba) ni muislamu sana na sioni aibu kusema mimi ni muislamu, tena ni muislamu sana,” baada ya maneno hayo Maalim Seif alisema, amani ina thamani.
Kwa kauli yake, Maalim Seif alikuwa na vitu viwili mkononi, Mosi; aingie madarakani kwa damu ya Wazanzibar kwa kuwa walikuwa tayari ama atumie njia ya amani kupata alichotaka ‘amani ina thamani.’
Fatma alitambua Maalim Seif alitawala nyoyo za Wazanzibari. Aliamini pale walipofika, ilibaki kauli ya Maalim Seif pekee Zanzibar igeuke kuwa bahari ya damu. Maalim Seif alijua, kwa kauli yake kweli Zanzibar ingekuwa bahari ya damu, lakini kwake amani ni zaidi ya chochote.
Alijua ndani ya ardhi ya Zanzibar ana watoto, ana wajukuu, vitukuu, wapwa, binamu, viongozi wake wa dini na ndugu wengine. Kwa fikra za Maalim Seif, vyote hivi aliona kuwa na thamani zaidi kuliko kuingia Ikulu ya Zanzibar kwa damu.
Maalim Seif na wafuasi wake licha ya kuamini katika chaguzi zote alizoshiriki kama mgombea urais wa Zanzibar – 1995, 2000, 2005, 2010, 2015 na 2020 alishinda, hakuwahi kuamini katika vurugu, huo ndio upekee wake Afrika mpaka leo.
Kwa umri wa Maalim Seif na maeneo aliyopita kama kiongozi katika nchi za Afrika na Dunia, alitamani amani zaidi ya vurugu. Kutokana na kile kinachochagizwa na wachache nchini, narejea kauli ya Maalim Seif kwamba ‘AMANI INA THAMANI.’