Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imesema kuanzia Februari, 2021 hadi Machi 2025, imefanya kaguzi 275 katika kuhakikisha usalama wa huduma ya reli nchini.
Kaguzi hizo zimehusisha miundombinu, vichwa vya mabehewa na uendeshaji, ambapo kati ya kaguzi hizo, 143 zilikuwa za Shirika la Reli Tanzania (TRC) na 132 zilikuwa za Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).
Mkurugenzi Mkuu wa LATRA Habib Suluo, alitoa kauli hiyo leo April 14, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Wahariri na Waandishi wa Habari kwa ajili ya kuelezea mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu, Hassan.
Suluo alisema, katika maandalizi ya kuanza kwa huduma za usafiri wa abiria kwa kutumia SGR, LATRA ilikuwa na jukumu la kuthibitisha ubora wa vitembea reli kabla ya kuanza kutoa huduma.
“LATRA iliungana na timu ya watalaamu wa TRC na Wizara ya Uchukuzi kwenda nje ya nchi (zilizokuwa zinaunda mebehewa) na kukagua kuthibitisha jumla ya vichwa vya treni 17, mabehewa ya abiria 56, treni za seti za umeme (EMU) 10 na mabehewa ya mizigo 264,” alisema Suluo.
Alisema, kaguzi hizo zilifanyika kwenye nchi za Korea, China, Malaysia na Ujerumani “Pia, mamlaka imefanya kaguzi za majaribio kwa mabehewa ya vichwa hivyo baada ya kuwasili nchini kabla ya kuanza kutoa huduma.”
Aidha, alisema mbali na kaguzi hizo, katika mwaka wa fedha 2023/2024, LATRA ilitekeleza jukumu la kisheria chini ya Kifungu cha 5(1)(C) kwa kupanga nauli za daraja la uchumi (Economy class) wakati wa uanzishwaji wa huduma za treni ya Kisasa (SGR).
“Kwa mujibu wa kifungu cha 19 cha Sheria ya LATRA, Bodi ya Wakurugenzi iliidhinisha nauli za abiria kwa daraja la uchumi kwa treni inayosimama kila kituo na treni inayosimama vituo maalum na kuanza kutumika Juni 2024,” alisema Suluo.