Na Peter Lyowa
KLABU ya Yanga leo wanawakaribisha watani wao wa jadi Simba kwenye uwanja wa Mkapa kwenye mchezo wao wa Ligi Kuu ya NBC, ingawa miamba hawa wanapokutana mechi yao inakuwa tofauti na michezo mingine ya Ligi.
Miamba hao wa soka nchini Tanzania, wanaingia uwanjani kila mmoja akiwa na matumaini makubwa ya kuondoka uwanjani na pointi tatu muhimu, huku wachambuzi na mashabiki wa soka wakijivunia rekodi za makocha wao; Juma Mgunda (Guardiola Mnene) wa Simba na Nasreen Nabi (Profesa) wa Yanga.
Ukiwasikiliza wachambuzi wengi na mashabiki, macho yao yameelekezwa zaidi kwa kocha wa Simba, ambaye ndio mechi yake ya kwanza kukabiliana na Yanga tangu alipokabidhiwa kikosi hicho kilichokuwa chini ya Zoran Maki ambaye mkataba wake ulivunjwa baada ya makubaliano ya pande mbili (Simba na kocha huyo).
Mgunda ambaye alikuwa kocha Mkuu wa Coastal Union, alianza kibarua chake Simba alipofunga safari kuelekea nchini Malawi kukabiliana na ‘Nyasa Big Bullet’ na kushinda 2-0, kisha Simba ikarudi nchini na kupapatuana na Prisons kwenye mchezo wa Ligi Kuu ambapo walishinda 1-0 na kunyakua pointi tatu.
Mara baada ya mechi hiyo, Simba walivaana tena na Nyasa Big Bullets jijini Dar es Salaam kwenye mechi ya marudio, na wakaibuka wababe kwa mabao 2-0 na wakafuzu Raundi ya Kwanza na baadaye wakacheza na Ligi Kuu dhidi ya Dodoma Jiji na kushinda mabao 3-0.
Simba katika harakati za kujinoa zaidi, wakafunga safari kwenda Visiwani Unguja, ambako walicheza mechi mbili ambazo zote walishinda; mechi ya kwanza walicheza na Malindi ambapo walishinda 1-0, na mechi ya pili waliwafunga Kipanga mabao 3-0.
Mara baada ya mechi hizo, Simba walifunga safari kuelekea nchini Angola kuwakabili Primeiro de Agosto katika mechi ya kwanza ya Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambako walishinda mabao 3-1 na kwenye mchezo wa marudiano uliofanyika kwenye Uwanja wa Mkapa, Simba walishinda 2-0 na kufuzu hatua ya makundi huku wakiwa na rekodi nzuri kwenye mechi zake za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kutokana na hilo, mashabiki wengi wa Simba wana matumaini makubwa ya kushinda kwenye mechi ya leo dhidi ya watani wao wa jadi, na wana matumaini makubwa na Mgunda na kwenye mitandao ya kijamii na hata mitaani, wanaonekana kushinikiza kocha huyo akabidhiwe kikosi hicho moja kwa moja.
Kwa upande wa kikosi cha Yanga, ambacho kinanolewa na Nabi, ambaye mashabiki wa klabu hiyo wanamuita Profesa, nao wanapata jeuri ya kushinda mchezo huo kutokana na rekodi nzuri dhidi ya watani wao wa jadi, huku wakijivunia matokeo waliyoyapata kwenye mchezo wa ngao ya Jamii na mechi ya mwisho ya Ligi waliyoshinda 2-1 dhidi ya Simba.
Mbali na hilo, ubingwa wa Ligi Kuu 2021/2022 ambao waliupata na kuweka rekodi ya kucheza mechi 39 bila kufungwa na mwendelezo mzuri wa mechi za Ligi Kuu msimu wa 2022/2023, ambapo hadi sasa hawajapoteza mchezo wowote, nao unawapa matumaini makubwa ya kushinda derby hiyo, huku wakijitapa kwamba wana kikosi kilichosheheni kuanzia golini hadi safu ya ushambuliaji sambamba na uwezo mkubwa wa benchi la ufundi.
Kwa upande mwingine Yanga wana changamoto inayoshusha morali baadhi ya mashabiki wake, ambapo kushindwa kufuzu kuingia kwenye hatua ya makundi baada ya kutolewa na Al Hilal ya Sudan, kumewafanya waamini mchezo wa leo unaweza kuwa mgumu kwao.
Hata hivyo, licha ya changamoto hizo bado mchezo huo unatarajiwa kuwa mzuri na wenye ushindani mkubwa kama ilivyo kawaida pindi timu hizo zinapokutana, ambapo taarifa zinaonyesha kuwa, Simba na Yanga ni miongoni mwa derby kubwa barani Afrika (Kariakoo derby) na timu hizo zina mashabiki kila kona ya dunia.
Mechi nyingine zinazofanana na hiyo inapatikana nchini Afrika ya Kusini kati ya Orlando Pirates dhidi ya Kaizer Chiefs ambayo inajulikana kama ‘Soweto derby’. Nyingine ipo nchini Morocco kati ya Wydad Casablanca dhidi ya Raja Casablanca nayo ni maarufu kama ‘Casablanca derby’.
Nchini Misri kuna ‘Cairo derby’ inayowakutanisha Al Ahly dhidi ya Zamalek. Tunisia kuna ushindani mkubwa kati ya Club Africain na Espérance Sportive de Tunis. Kenya kuna derby maarufu kwa jina la ‘Mashemeji derby,’ inayowakutanisha Gor Mahia na AFC Leopards.