Kura za CCM hizi hapa

0

Na Albert Kawogo

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimezindua rasmi mchakato wa Kampeni za kuwania Urais, Ubunge na Udiwani na tayari kampeni hizo kwa upande wa Urais zimeanza kuchukua sura nyingine baada ya Mgombea wake Dkt. Samia Suluhu Hassan kuanza kuinadi ilani ya uchaguzi ya 2025/2030 kwa kishindo katika mikoa ya Morogoro na Dodoma.

Chama hiki tawala, kinaingia kwenye uchaguzi huku kikijivunia mtaji mkubwa wa kazi zake katika kipindi cha miaka mitano.

Pia, CCM kinaingia kwenye uchaguzi kikitamba kujiimarisha zaidi kwenye ngome zake muhimu ambazo kimekuwa kikizoa kura nyingi.

Kimsingi, turufu kubwa ya CCM inaangaziwa Mikoa ya Kanda ya Ziwa, kwani ndiyo inayobeba idadi kubwa ya watu pamoja na Kanda ya Mashariki, Nyanda za Juu Kusini na Kanda nyingine.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, mikoa sita pekee ya Kanda ya Ziwa inabeba watu 16,687,560 ikiongozwa na Mwanza yenye watu 3,966,872.

Mikoa ya Kanda hiyo ukiacha Mwanza; ni pamoja na Geita, Simiyu, Shinyanga, Mara na Kagera ambapo kuna asilimia kubwa ya wapenzi, wanachama na mashabiki wa CCM.

Kati ya mikoa hiyo, Rais Samia ana uhakika wa kuzoa kura kwa kuwa kwenye maeneo hayo, ilani ya CCM imetekelezwa kwa sehemu kubwa ikiwemo miradi ya maji, kusaidia, wavuvi wanaoendesha shughuli zao ziwa Victoria ikiwa ni pamoja na kuwapatia boti za uvuvi.

Rais Samia pia alisaidia vijana, ujenzi wa vizimba ili wanufaike na uchumi wa buluu uliopo kwenye ukanda wa Ziwa Viktoria.

Awamu ya kwanza ya mradi huu ilianza mwaka wa fedha 2022/2023 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 11.5, ambapo pia boti 160 zilikopeshwa kwa wanufaika 3,163.

Lengo la boti hizo ni kusaidia kuongeza uzalishaji wa mazao ya uvuvi, kudhibiti uvuvi haramu huku vijana 113 kutoka Mkoa wa Tanga, ambao hapo awali walijihusisha na uvuvi haramu, wameamua kubadili maisha yao na sasa wanajiunga na vikundi vya uvuvi halali kupitia mpango huu wa mikopo nafuu.

Naye Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA), John Bina, anasema, wachimbaji wadogo wa madini nchini wameazimia kwa kauli moja kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan, kutokana na mchango wake mkubwa katika kuinua sekta ya wachimbaji wadogo.

Ushahidi wa hicho anachosema, ni kitendo cha wachimbaji wadogo kuichangia CCM Shilingi Bilioni 16 ili kufanikisha jambo lake.

Dkt. Samia pia amesaidia kwa kiwango kikubwa kutatua tatizo la miundombinu ya barabara, umeme, huduma za kisheria, afya, elimu, maji na ufugaji. Yapo mengi.

Kanda ya Mashariki ni ya pili kwa wingi wa watu. Kanda hiyo pekee ina watu 12,630,726 ikiongozwa na Dar es Salaam yenye idadi kubwa ya wakazi. Kanda hiyo ndio jicho muhimu kwa CCM kuhakikisha inazoa kura za kutosha.

Mkoa wa Dar es Salaam pekee una watu 5,383,728. Mikoa mingine inayojenga Kanda hiyo ni pamoja na Morogoro na Pwani.

Kama ilivyo Kanda ya Ziwa, sehemu kubwa ya miradi imekamilika huku miundombinu ya barabara ikiwekwa sawa. Hapa ndipo mashabiki wa CCM wanasema “Hatuna Deni Na Mama.”

Rais Samia ameigusa mikoa hiyo kwa huduma mbalimbali za kijamii na ni maeneo machache yaliyosalia ambayo yanaendelea kufanyiwa kazi na anasubiri ridhaa ya mitano mingine ili akamilishe.

Kanda nyingine inayobeba idadi kubwa ya watu ni Nyanda za Juu Kusini ambayo inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na idadi kubwa ya wakazi.

Kanda hiyo yenye mikoa ya Mbeya, Songwe, Ruvuma, Rukwa, Njombe na Iringa inashika nafasi ya tatu ikiwa na watu 9,160,428 ambao ziko asilimia kadhaa za kura za CCM.

Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ni kati ya maeneo ambayo Rais Samia ametekeleza mambo mbalimbali kupitia Ilani katika ukanda huo unaosifika hasa kwa kilimo. Ukanda huo ndio unaolisha Tanzania na Afrika.

Mikoa hiyo imefanya ukuaji wa sekta ya kilimo kuongezeka kutoka asilimia 2.6 mwaka 2021 hadi asilimia 4.2 mwaka 2023 huku Serikali ikilenga kufikia asilimia tano mwaka 2026 na asilimia 10 ifikapo 2030.

Aidha, kwa sehemu kubwa ukanda huo umefanya thamani ya mauzo ya mazao ya kilimo nje ya nchi kuongezeka kutoka Dola Bilioni 1.2 mwaka 2019/2020 hadi Dola Bilioni 3.54 mwaka 2023/2024.

Hili ni ongezeko la zaidi ya mara mbili katika kipindi kifupi hatua inayoonyesha Tanzania inatambulika si kwa utalii pekee, bali pia kwa ubora wa mazao yake ya kilimo duniani.

Uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kwa kiwango kikubwa kutoka tani Milioni 17.14 mwaka 2021/2022 hadi tani Milioni 22.80 mwaka 2023/2024. Sasa Watanzania hawazungumzii tu kuhusu usalama wa chakula, bali pia nafasi ya kuisambaza Afrika Mashariki na hata nje ya bara. Ndoto ya Tanzania kuwa ‘food basket’ wa ukanda huu, si hadithi tena ni mwelekeo wenye uhalisia.

Kwa upande wa mahindi, Tanzania sasa ni mzalishaji wa pili kwa ukubwa barani Afrika. Kutoka Tani Milioni 6.4 mwaka 2021 hadi tani Milioni 12.26 mwaka 2023/2024. Wakulima hawahitaji tena kusubiri miujiza ya mvua au huruma ya madalali, sasa wana uhakika wa pembejeo, elimu ya ugani, na masoko ya uhakika.

Hayo yote ni kutokana na Rais Samia kukubali kuweka fedha nyingi katika bajeti ya kilimo, Shilingi Trilioni 1.2 za Wizara hiyo.

Eneo hili linagusa Kada nyingi ikiwemo mafunzo ya maofisa ugani, ununuzi wa pembejeo, mbegu na ujenzi wa mtandao wa maji kwa ajili ya umwagiliaji.

Kura nyingine ambazo CCM inatarajia kuzoa ni Kanda ya Kaskazini ambayo ina idadi ya watu 8,726,288 huku mkoa wa Tanga ukiongoza kwa idadi kubwa ya watu. Mkoa huo una watu 2,615,597 ambao kwa sehemu kubwa ni ngome ya CCM.

Mikoa mingine inayounda kanda hiyo ni pamoja na Arusha inayoshika nafasi ya pili kwa idadi kubwa ya watu ikifuatiwa na Manyara wakati mkoa wa Kilimanjaro unashika nafasi ya mwisho kwa kuwa na idadi ndogo ya watu.

CCM ina nafasi kubwa kupenya hasa mkoa wa Arusha kwa kuzoa kura za kutosha baada ya kufanikiwa kuusambaratisha upinzani. Mkoa wa Arusha ulikuwa ngome ya upinzani hasa Chadema ambao mwaka huu hawamo.

Kanda ya Kati inayounda Mikoa ya Dodoma na Singida ni wazi inafahamika kuwa ni ngome ya CCM kwa muda mrefu kwamba haina presha kubwa ya kuzoa kura miongoni mwa watu 5,093,683. Kwa muda mrefu, CCM imekita mizizi yake Dodoma na ndio Makao Makuu ya nchi.

Mikoa ya Kanda ya Ziwa Magharibi inayoundwa na Kigoma, Tabora na Katavi na yenyewe inakaribiana na Kanda ya kati. Mikoa hiyo inakusanya watu 5,697,595.

Maeneo hayo, kwa sehemu kubwa Rais Samia ametekeleza Ilani hivyo ni wazi ameshazitengeneza kura za CCM miongoni mwa watu hao. Mikoa ambayo CCM inaweza kupata upinzani kiasi ni Mikoa ya Kusini ambayo idadi kubwa ya watu ni kama imegawanyika.

Mikoa hiyo ina mtawanyiko wa watu 2,828,975 ikiwa ni idadi ndogo kulinganisha na mikoa mingine. Lindi na Mtwara ndiyo mikoa pekee inayounda Kanda ya Kusini.

Pamoja na hayo, Mikoa hiyo inajivunia utekelezwaji wa Ilani ikiwemo huduma mbalimbali za kijamii kutoka Serikali ya Awamu ya Sita kama; maji, elimu, umeme, huduma za afya, barabara, Bandari.

Hivi karibuni, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika moja ya mikutano yake na wananchi wa mikoa ya Kusini alisema wananchi wa mikoa ya Kusini ikiwemo Ruangwa hawana deni na wanasubiri kutiki ifikapo Oktoba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here