Kuendelea kubaki chini, sio haki yako

0

Na Abel Kiharo

MAMA huyu, baada ya kujifungua mtoto wake, alijikuta katika majonzi na machungu makali zaidi, huku akiogopa hata kumuangalia mtoto huyo aliyembeba tumboni miezi tisa.

Hali hii ilimtokea mama huyu, baada ya kugundua kuwa, amemzaa mtoto ambaye hakuwa na miguu wala mikono, mtoto huyu ndiye Nicholas James Vujicic, ambaye wengi wetu tunamfahamu kama Nick Vujicic.

Kuzaliwa bila mikono wala miguu, haikuwa sababu ya Nick kushindwa kufanya mambo makubwa maishani mwake. Kwake, ameitumia hali yake hiyo kama kichocheo cha kufanya mambo makubwa na kuendelea kugusa maisha ya walio wengi duniani.

Bila kuwa na miguu wala mikono, Nick ameandika zaidi ya vitabu vitano, anazunguka ulimwenguni kote akiihubiri injili na kuwahamasisha watu, ni mjasiriamali na mwanzilishi wa shirika lisilo la kiserikali la ‘Life Without Limbs’.

Nick Vujicic haioni hali aliyonayo, kama kisingizio cha kutokuzipigania ndoto zake, yeye ameamua hali hiyo, liwe ni daraja la kumfikisha kwenye ndoto zake.

Baada ya kuyasoma maisha ya Nick Vujicic, kwa kupitia vitabu vyake, nilijikuta napatwa na aibu. Hali hii ilinitokea baada ya kugundua kuwa, nimeishi maisha yangu yote kwa visingizio na kulalamika tu.

Hapo ndipo mtazamo wangu juu ya maisha ulipoanza kubadilika, nikaona kumbe zile sababu zangu zote, ambazo nimekuwa nikizitoa kama visingizio vya kushindwa kuzipigania ndoto zangu, hazikuwa na mashiko yoyote!

Kama Nick ameweza kuziishi ndoto zake bila kuwa na miguu wala mikono, kwanini mimi na wewe tushindwe kuziishi ndoto zetu? Kweli, ikiwa ndugu yetu huyu ameweza, basi mimi na wewe hatuna hoja zozote zenye nguvu, tunazoweza kuzitoa mbele za watu kama sababu zilizosababisha tushindwe kuishi maisha makubwa.

Unazikumbuka enzi zetu za utoto? Bila shaka unaikumbuka ile mipango mikubwa, tuliyokuwa nayo utotoni. Tukiwa watoto tuliwaza mawazo makubwa siku zote na tuliamini siku tukiwa wakubwa, tutakuwa na uwezo mkubwa wa kuyaweka kwenye uhalisia mawazo hayo.

Hatukuamini katika kushindikana, hatukuamini katika uhaba wala ubinafsi. Siku zote tuliamini katika uwezekano, utoshelevu (utele) na utoaji.

Tukiwa watoto tuliamini, kikwazo kikubwa kilichokuwa kikituzuia kupata kitu chochote kikubwa na bora tulichokihitaji maishani mwetu ni utoto tu. Na siku tukiwa wakubwa, kikwazo hicho kisingekuwepo tena, hivyo tungeyapata yale yote mazuri ambayo tumetamani tuwe nayo maishani mwetu. Sasa tumeufikia ukubwa ule tuliousubiri kwa hamu sana, ni kwanini yale matarajio yetu yameyeyuka mfano wa barafu juani?

Pasi shaka, kila mmoja anazo sababu zake ambazo anaziona kuwa, ndizo zilizopelekea aendelee kuishi maisha yaleyale ya chini siku zote. Sababu hizo zitakuwa ni pamoja na ukosefu wa fedha, elimu kubwa na ndugu wa kusaidia.

Hizo ndizo zile sababu ambazo, watu wengi huamini ndicho chanzo kikubwa kilichopelekea washindwe kuyaishi yale maisha makubwa ambayo, wamekuwa wakitamani kuyaishi tangu utotoni.

Ninalo neno kwako, msomaji wangu mpendwa! Kinachochangia ushindwe kupiga hatua kubwa maishani, si ukosefu wa fedha, elimu kubwa au ndugu wa kukusaidia; kinachofanya ushindwe kupiga hatua maishani mwako si kingine bali ‘visingizio’.

Kwa lugha ya Kiingereza huitwa ‘excuses’, yaani zile sababu alizonazo mtu ambazo, zinamfanya aamini kuwa, anayo haki ya kutokufanya mambo makubwa au kupiga hatua zaidi maishani mwake.

Hizi ni zile sababu zinazompatia mtu ujasiri, wa kujitetea ili aonekane yuko sahihi kabisa, kuendelea kuwa masikini, kutokufika mbali kielimu na kutokufanya mambo makubwa maishani mwake kwa ujumla.

Ngoja nikung’ate sikio kidogo msomaji wangu; Pale unapotaka kuanza kulitekeleza jambo, usikimbilie kutafuta sababu zitakazokufanya ujione kama mtu asiye na uwezo wa kulifanya jambo hilo.

Kimbilia kwanza kwenye zile sababu zinazokuthibitisha wewe, kama mtu mwenye uwezo mkubwa wa kulitekeleza jambo hilo. Usianze kwa kutafuta sababu zitakazokuonesha, kwanini ushindwe kupiga hatua yoyote maishani mwako, anza na zile sababu zitakazokuonesha kuwa, unapaswa na unastahili kabisa kuwa katika hatua za juu zaidi ya hapo ulipo sasa.

Siku zote visingizio ni vingi, kwahiyo kama utakuwa umeamua kuvitafuta, kwa hakika utavipata vya kukutosha! Hata hivyo, mara zote visingizio vitakufanya uamini unayo haki ya kusalia kuwa hapohapo ulipo sasa. Hata siku moja haitatokea, visingizio ulivyonavyo ikawe sababu ya wewe kupiga hatua mbele kimaisha.

Mfano; Zile sababu unazozitoa ili uonekane umestahili kuwa masikini mpaka hivi leo, ni lini sababu hizo zitakusaidia kuondokana na umasikini huo ulionao? Kwanini usizitafute sababu zitakazokufanya ujione kama mtu, usiye na haki hata kidogo ya kuendelea kuwa masikini?

Zile sababu ulizonazo zinazokuonesha kuwa, haukuwa chanzo cha kufanya vibaya kwenye mitihani yako, ni lini sababu hizo zitakapo kusaidia kufanya vizuri katika mitihani yako ijayo?

Visingizio (sababu za kujitetea) siku zote, hukufanya uamini unayo haki ya kuendelea kuishi maisha ya viwango vya chini. Sababu hizi, hukufanya uamini uko sahihi kabisa kujiita ‘asiyeweza’ ‘masikini’ ‘asiye na akili darasani’ ‘asiye na mtaji’ ‘aliye duniani kuhangaika’ n.k.

Kwenye maisha, ili uweze kuvifikia viwango vya juu, ni lazima uhakikishe umeuvuka msatari huu wa visingizio. Tofauti na hapo, maisha yako yatasalia kuwa katika viwango vilevile (vya chini) siku zote.

Kibaya zaidi kuhusu visingizio ni kwamba, hufanya iwe ni rahisi kuukimbia wajibu wako, juu ya maisha yako mwenyewe. Hali hii inakufanya uwe ni mtu wa kulalamika, kuwalalamikia ndugu, jamaa na marafiki, kuilalamikia serikali yako na mazingira yote yaliyokuzunguka.

Unachopaswa kujua ni kwamba, mtu muhimu zaidi unayemhitaji katika maisha ili uweze kupiga hatua kubwa kuelekea kwenye viwango vile vya juu kimaisha; ni wewe mwenyewe kwanza. Wewe ndiyo sababu ya kujengwa kwa maisha yako au kubomolewa, kuinuliwa zaidi au kushushwa.

Kama ukiwa ni mtu wa visingizio, utaiona dunia hii kama sehemu iliyojaa matatizo mengi, lakini kama utauvuka mstari huu wa visingizio, hatimaye ukawa ni mtu wa kuyakubali majukumu na kuwajibika, utaiona dunia hii kama sehemu iliyofurikwa na fursa nyingi zaidi.

Ukiwa ni mtu wa visingizio, utawakosa hata watu bora wa kushirikiana nao, kwa kuwa hayupo mtu bora apendaye kushirikiana na mtu aliyetawaliwa na visingizio, lawama na kujikatia tamaa.

Ukiwasoma wale wote waliopiga hatua kubwa kwa kupitia yale wayafanyayo, moja ya sifa kubwa utakayoikuta ndani ya kila moja ni hii: Si watu wa visingizio (excuses).

Ikiwa na wewe unayo ndoto ya kufika mbali kimaisha, hakikisha unauvuka mstari huu wa visingizio. Yapende majukumu, furahia uwajibikaji na jifunze kuamini zaidi katika utele.

*Mwandishi wa makala hii ni Mkufunzi wa Vijana, Mwandishi na Mjasiriamali. Kwa maoni, ushauri au maswali, usisite kuwasiliana nae kwa anuani zifuatazo:- Simu: 0767180002/0628733839, Baruapepe: kiharoabel@yahoo.com na WhatsApp: 0767180002.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here