☑️ Kiwanda kina uwezo wa kuzalisha tani 5 hadi 8 kwa saa.
📍 Tanga
KIWANDA cha Tansalt kilichopo mkoani Tanga kimekuwa msaada mkubwa kwa wachimbaji na wakulima wa chumvi nchini kwa kusaidia kuwapatia uhakika wa soko la bidhaa hiyo, hatua ambayo imechangia kuongeza kipato cha wazalishaji wadogo na kukuza thamani ya chumvi katika masoko ya ndani na ya kikanda.
Hayo yalibainishwa na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa Tanga, Mhandisi Laurent Bujashi wakati akizungumza na Madini Diary ambapo alieleza kuwa, wachimbaji wa chumvi wamekuwa wakikumbana na changamoto ya kuyauza mazao yao kwa bei ya kusuasua kutokana na ukosefu wa soko la uhakika.
Hata hivyo, kupatikana kwa Tansalt kumeimarisha mnyororo wa thamani wa chumvi, kwani kiwanda kinanunua na kuchakata chumvi ghafi kutoka kwa wachimbaji wadogo wa Tanga na mikoa ya ukanda wa pwani na kuisambaza kwa wingi katika masoko ya kitaifa na nje ya nchi.
“Mbali na kuongeza thamani ya chumvi, kiwanda hicho pia kimetoa ajira kwa wakazi wa Tanga na kuchochea shughuli nyingine za kiuchumi, ikiwemo usafirishaji, biashara ndogo ndogo na huduma za kijamii. Vilevile, uwepo wa chumvi yenye iodini inayozalishwa na Tansalt umechangia kwa kiasi kikubwa katika mapambano dhidi ya maradhi yatokanayo na upungufu wa madini ya iodini nchini.” alisema Bujashi.
Kwa mujibu wa wadau wa sekta ya chumvi, Tansalt inatajwa kuwa mfano wa jitihada za Serikali na sekta binafsi katika kuhakikisha rasilimali za bahari na ardhi zinachangia moja kwa moja kwenye maendeleo ya wananchi, huku ikihimiza uwekezaji zaidi katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata chumvi ili kupanua masoko.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kiwanda hicho, Badru Issa Badru alisema kuwa, Kiwanda kinazalisha chumvi kwa matumizi ya nyumbani (domestic salt), viwandani (industrial salt), pamoja na chumvi yenye madini ya iodini kwa ajili ya afya ya binadamu (iodized salt).
“Tansalt imejipanga kuhakikisha wachimbaji na wakulima wa chumvi nchini wanapata soko la uhakika kwa bidhaa zao. Tunachakata chumvi ghafi kutoka kwao na kuisambaza kwa viwango vya kitaifa na kikanda, hatua inayoongeza kipato cha wananchi na kuchochea maendeleo ya uchumi wa Tanga na taifa kwa ujumla. Kiwanda kina uwezo wa kuzalisha tani 5 hadi 8 za chumvi ndani ya saa moja,” alisema Badru.
Aidha, aliongeza kuwa Tansalt ni moja ya wazalishaji wakubwa nchini, na chumvi yake inasambazwa ndani ya Tanzania na pia kuuzwa kwenye masoko ya Afrika Mashariki.