Kinana: Wanasiasa tumuunge mkono Rais Samia

0

*Asema ameonesha dhamira ya kweli kuleta mageuzi ya kisiasa

*Amkumbuka Maalim Seif, asema alikuwa mwanasiasa mahiri

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana amewataka viongozi wa vyama vya siasa nchini kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amedhamiria kuleta maridhiano na mageuzi ya uendeshaji wa siasa nchini.

Kinana aliyasema hayo jana wakati akiufunga mkutano wa pili wa kumuenzi Hayati Maalim Seif Sharif Hamad wenye maudhui ya elimu, ukuzaji vipaji, ubunifu na uwezeshaji, uliofanyika katika ukumbi wa Golden Tulip, kisiwani Unguja.

”Hii sio kazi rahisi kwani ziko changamoto zinazotukabili ikiwa ni pamoja na kutofautiana katika utekelezaji wake, kubishana kuhusu vipaumbele vyake na kuwa na mawazo tofauti kwa namna ya kasi ya utekelezaji wake,” alisema.

Kinana aliwataka wanasiasa nchini kuendeleza utamaduni wa kuzungumza, kushauriana na kila mmoja kuheshimu mawazo ya mwenzake licha ya tofauti za kimtazamo na kimkakati.

Alisema, Rais Samia ana lengo la kusimamia haki, kukuza na kuimarisha uhuru, kupanua wigo wa kuendesha shughuli za kisiasa na kuleta mageuzi katika uendeshaji wa serikali kwa madhumuni ya kuharakisha maendeleo ya nchi na watu wake.

Pia, Kinana alisema wanasiasa wote kwa pamoja wanapaswa kukubaliana kuhusu mambo muhimu yanayofanywa na Rais Samia kutokana na umuhimu wake kwa nchi na mustakabali wa taifa.

Alisema, katika kudhihirisha utayari wake katika kuleta mageuzi ya kweli ya kisiasa nchini, mwaka jana Rais Samia alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa kumbukumbu ya Maalim Seif ambapo Rais wa Zanzibar Dkt. Mwinyi na Rais Mstaafu Amani Karume walikuwa wageni mashuhuri katika mkutano huo.

Alisema, viongozi hao watatu ni viongozi wakuu ndani ya Chama hatua ambayo siyo ya kiitifaki bali ni tafsiri ya dhamira ya kweli ya kujenga mazingira mapya ya kisiasa na kijamii nchini.

Kinana alisema, jamii ya Watanzania inathamini haki, inajali uhuru na inajenga misingi ya kuheshimiana na kujenga umoja wa kitaifa.

KUHUSU MAALIM SEIF

Akimzungumzia Maalim Seif, Kinana alisema ni kiongozi aliyekuwa na sifa nyingi nzuri zinazomfanya kuwa mtu mwenye maono, msimamo, subira, mpenda haki, mwanamapinduzi na mwenye ushawishi.

Alisema, Maalim alipenda kuona vijana wanapata elimu bora iliyolingana na mahitaji ya wakati na yenye kuwajenga vijana kudadisi, kujituma, kujitegemea na kuwa wazalendo kwa nchi yao.

Aidha, aliamini kwa dhati kuwa elimu ndiyo mkombozi wa kweli kwa mwanadamu ndio maana elimu yake ya msingi na ya juu aliipata kwa kujituma bila kukata tamaa.

Kwa mujibu wa Kinana, ndiyo maana viongozi wa wakati huo waliona na kuthamini kiu ya Maalim Seif jambo lililofanya apewe nafasi ya kuongoza Wizara ya Elimu akiwa na umri mdogo.

“Jukumu hilo lilikuwa zito kwa kuwa fursa za elimu zilikuwa ndogo na hafifu, kwa ujasiri mkubwa na kwa hatua za kuthubutu alijitwisha dhamana ya kufanya kazi aliyopewa kwa ustadi, hasama na ari kubwa,” alisema.

Alieleza kuwa, kutokana na juhudi zake vijana wengi wa Zanzibar walipata nafasi za elimu ndani na nje ya nchi, ambapo Maalim aliamini katika elimu, nafasi ya elimu na fursa zinazotolewa na elimu katika maisha ya binadamu na uhai wa taifa.

“Nafurahi kuona kwamba siku ya leo (jana) tumejumuika hapa kujadili umuhimu wa elimu, ubunifu, ukuzaji vipaji na kutafakari kuhusu elimu, nafasi, umuhimu, msukumo wake, mahitaji ya kipindi hiki na uhusiano wa elimu na msukumo wa maendeleo kwa Tanzania na duniani,” alisema.

Alieleza kuwa, kwa kutambua hayo yote, Tanzania iko katika mchakato wa kutazama upya sera na mfumo wa elimu kwa lengo la kuboresha elimu ili elimu wanayopatiwa watoto ilenge kujenga, kujitegemea na kuendana na mabadiliko na mahitaji ya dunia ya sasa.

Alisema, mada zilizojadiliwa katika mkutano huo zimejadili umuhimu wa elimu, sera na namna inavyotakiwa kuikomboa jamii na kuharakisha maendeleo yao hususan katika zama hizi za utandawazi na maendeleo ya teknolojia.

Makamu mwenyekiti Kinana alifafanua kuwa, amekuwa akifuatilia na kuridhishwa na namna vijana wengi wanavyojituma kujielimisha kwa kutumia akili na nguvu zao pamoja na ubunifu katika kujitafutia fursa za kujitengenezea ajira, kujiongezea kipato na kuwa wabunifu.

“Hata tumeyaona katika nyanja za teknoloji, sanaa, biashara na katika uzalishaji wa mazao na bidhaa, vijana wetu wanajituma na wanahangaika kutafuta njia kadhaa za kujiajiri na kujiongezea kipato, wanabuni majibu kwa mahitaji ya jamii na kuchangia maendeleo ya taifa letu,” alisema.

Alisema, vijana wanastahili kupongezwa kwa namna wanavyojituma na kusema kuwa inadhihirisha kuwa wakati mwafaka umefika wa kuweka mkazo mkubwa katika elimu inayowaandaa watoto kutumia akili na nguvu zao ili kupata na kujiongezea kipato.

Alisisitiza kuwa, kunahitajika utafiti kwa kuchambua kazi za ubunifu zinazofanywa na vijana wa Tanzania, changamoto wanazozipata, kasoro na upungufu wanaokabiliana nao.

Alisema, kwa kufanya hivyo watapata baadhi ya majibu katika kukabiliana na upungufu katika elimu ya Tanzania yanayosababisha vijana kukumbana na vikwazo mbalimbali.

Hivyo, alitumia fursa hiyo kuwashauri kwa wale wanaofanya tathmini ya uboreshaji wa elimu nchini ili wapate nafasi ya kuwasikiliza vijana wa vijijini na mijini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here