KATIBU wa Itikadi, Siasa na uenezi CCM Taifa Kenani Kihongosi amewataka watanzania kuwapuuza wanasiasa ambao wamekuwa wakichochea kuvuruga Amani iliyopo nchini ambayo ni Tunu kwa Taifa letu.
Kihongosi ameyaeleza hayo leo Septemba 6, 2025 Mkoani Iringa kwenye mkutano wa kampeni ya mgombea wa Urais kwa tiketi ya chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika Jimbo la Kalenga ukijumuisha majimbo ya Kalenga na Isimani wilayani Iringa mkoani humo, Kihongosi alisema wapo wanasiasa ambao wanajipanga kuleta vurugu siku ya kupiga kura Oktoba 29 huku wakiwahamasisha vijana kutekeleza vurugu hizo ili kuvuruga uchaguzi.
“Ninapenda kuwasihi vijana na wananchi kwa ujumla kuwa tuwakatae wale wote wanaochochea vurugu nchini,kwani hawaitakii mema nchi yetu, vijana hakikisheni mnajibidiisha katika shughuli za uzalishaji. Tumieni muda wenu mwingi kujiingizia kipato ikiwemo kijikita katika kilimo ili kujikwamua kiuchumi,” alisisitiza Kihongosi.