HALMASHAURI ya Wilaya ya Kibaha imevuka lengo la ukusanyaji mapato kwa asilimia 110 na kufanikisha utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Regina Bieda, wakati wa kikao maalum cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Juni 16, 2025 kwa ajili ya kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Bieda alisema, mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano mzuri kati ya wataalamu wa Halmashauri, Baraza la Madiwani pamoja na wananchi, na kwamba usimamizi madhubuti umeiwezesha Halmashauri hiyo kupata hati safi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, alipongeza Halmashauri ya Kibaha kwa kazi nzuri ya ukusanyaji mapato na utekelezaji wa miradi, akisema:
“Niwapongeze, mnafanya vizuri sana kwenye mapato na usimamizi wa miradi. Sasa nawataka msizalishe hoja kabisa.”

Kunenge alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuchapa kazi kwa kuzingatia falsafa ya R5 ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku akiitaka Halmashauri kupanga mji kwa weledi kutokana na ukuaji wake wa kasi na mvuto kwa wawekezaji.
Naye Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Mkoa wa Pwani Pastorine Massawe alipongeza Halmashauri hiyo kwa kujibu hoja 20 kati ya 29 zilizoibuliwa na kubakiza hoja 9 tu za kisera, huku akiitaka kuhakikisha haina hoja mpya katika ukaguzi ujao.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Halima Jongo, alitumia fursa hiyo kumshukuru Mkuu wa Mkoa kwa ushirikiano na kumpongeza Mkurugenzi Bieda kwa uongozi bora na ushirikiano wake na baraza la madiwani.
