MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Erasto Makala, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kuipatia halmashauri hiyo fedha nyingi za miradi ya maendeleo.
Akizungumza leo, Februari 5, 2024, wakati wa mkutano wa Baraza la Madiwani la Robo ya Pili, Makala alisema, “Nichukue nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Rais wetu kwa kutuletea fedha nyingi za miradi na kwa kuteuliwa kuwa mgombea urais wa mwaka 2025.”
Katika hatua nyingine, Makala aliagiza maafisa maendeleo ya jamii kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa elimu, akibainisha kuwa baadhi ya wanafunzi wenye uwezo wa kufaulu wanashindwa kuendelea na masomo kutokana na shinikizo la wazazi wao, ambao wanawashinikiza kufeli ili waolewe au kwenda kuchunga mifugo.
Pia, Makala amewataka maafisa elimu kuandaa siku maalum ya wadau wa elimu kwa ajili ya kujadili changamoto zinazokwamisha maendeleo ya sekta hiyo na kutafuta suluhisho la pamoja.
Katika mkutano huo, Afisa Uchaguzi wa Wilaya, Garace Haule, alieleza kuwa maandalizi ya daftari la wapiga kura yanaendelea, ambapo kwa Mkoa wa Pwani, zoezi hilo linatarajiwa kuanza Februari 13 hadi 19, 2024.
Aliwataka madiwani kuhamasisha wananchi, hususan waliofikisha umri wa miaka 18, kujitokeza kujiandikisha kushiriki uchaguzi ujao.