‘Katika kulinda na kusimamia mazingira, kila mmoja anapaswa kuchukua hatua kwenye eneo lake’

0

WAZIRI Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema katika kusimamia na kulinda mazingira na kuhakikisha maendeleo endelevu kila mmoja anapaswa kuchukua hatua kwenye eneo lake.

Masauni amesema, katika juhudi za kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kuhifadhi viumbe hai, kuhimiza suala la matumizi ya nishati safi kwa ajili ya kupikia na maendeleo endelevu, haya yote hufanyika kwa ajili ya vizazi cha sasa na kinachokuja.

Ameyasema hayo wakati wa Iftar iliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Machi 22, 2025 jijini Dar es Salaam ambapo alisema, Ramadhani inatufundisha mambo mengi ikiwemo subira, huruma, na nidhamu pamoja na sifa njema.

“Tuendelee kushirikiana, kufanya kazi pamoja, na kufanya maamuzi ya pamoja ambayo yananufaisha mazingira na watu wanaoyategemea mazingira ambao kwa ujumla ni sisi wenyewe.

“Ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwa ushirikiano wenu, misaada mnayoendelea kutoa na juhudi zenu katika kazi hii kubwa na nzito ya kulinda mazingira.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Immaculate Sware Sesemi alisema, kuelekea Siku ya Kimataifa ya Kuondoa taka (International day of zero waste) NEMC inaandaa kuaidhimisha siku hiyo kuanzia Machi 28 hadi 30 Machi, 2025.

“Tukio hili lililopangwa kufanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, ni mahususi kwa kuyaleta pamoja makundi mbalimbali ya wadau wa mazingira kwa lengo la kuangazia umuhimu wa usimamizi endelevu wa taka na kukuza uchumi mzunguko (promote a circular economy),

“Kauli mbiu ya mwaka huu inasema “kufikia lengo la taka sifuri katika masuala ya mitindo na nguo” (“towards zero waste in fashion and textiles”) na kauli mbiu ya Kitaifa ni “TAKA NI FURSA”.

Alisema, hii itakuwa ni fursa nyingine nzuri watu kukutana tena na kuendelea kuimarisha ushirikiano katika kutafuta masuluhisho ya pamoja ya changamoto za kimazingira zinazotukabili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here