KARMA YA UONGOZI: Somo kwa wanaohamasisha maandamano

0

Na Mwandishi Wetu

NAJIULIZA maswali ya msingi, kama raia mwenye tafakuri na uzoefu katika uongozi. Je, wanaohamasisha maandamano ni wapinzani, wanaharakati, au ni watu wa ndani?

Jibu langu, nikiwa nimetazama kwa macho ya uzoefu, ni kwamba mara nyingi moto wa chokochoko huanzishwa na watu wa ndani, wale tuliowapa nafasi, tukawaamini, tukawasogeza, tukawalea, lakini wakalipa wema kwa usaliti.

Nilipokuwa kiongozi katika eneo fulani, niliamini katika mabadiliko yenye tija. Nilichagua njia ngumu ya kusema hapana kwa ubabaishaji, ulafi na matumizi yasiyo na maana kwa rasilimali za taasisi. Nilisimamia misingi, nidhamu, na uadilifu. Nilijua uongozi ni dhamana, si fursa ya kujinufaisha.

Lakini, hapo ndipo vita ilipoanza, vita isiyoonekana kwa macho, bali kwa vitendo, maneno na mikakati ya ndani. Wapo waliogeuza maendeleo kuwa tishio kwao, kwa sababu hayakuwahusu wao binafsi bali jamii pana.

Mikakati ya mapinduzi ilianza kimyakimya; fitna, majungu na upotoshaji vikaanza kumea mithili ya magugu kwenye shamba la mpunga. Nilipigwa vita na viongozi wenzangu wenyewe, na hata msaidizi niliyemsogeza katika ajira akanigeuka. Niliona ubinadamu wa kweli unavyopimwa katika upepo wa majaribu.

Ni viongozi watatu tu ndio walisimama nami. Walinifundisha maana halisi ya uongozi; kwamba kiongozi wa kweli hatetemeki anapopingwa kwa kufanya kilicho sahihi. Walinijenga kisaikolojia na kiroho, wakinipa mifano ya historia ya viongozi waliopitia mitihani mikubwa zaidi, lakini wakaendelea kusimama. Kwao, nitaendelea kuwa na heshima isiyo na kipimo, na ipo siku, nitawataja hadharani kama ushuhuda wa kwamba uongozi si tamasha, ni sadaka.

Nilipokuwa nimekata tamaa, nilitaka kujiuzulu. Nilihisi uchungu wa kutotambulika na waliokuwa wenzangu. Lakini, walinikumbusha maneno mazito: “Uongozi ni msalaba. Ukipendwa sana, ujue hujafanya mabadiliko; maana mabadiliko huumiza wenye faida katika mfumo wa zamani. Maneno haya yalinirejesha katika mstari wa imani yangu kwa Mungu na watu niliokuwa nawatumikia.”

Leo, ninapoona ushawishi wa maandamano, chokochoko, na propaganda za kisiasa, sishangai tena. Najua ya kwamba, mara nyingi watu wa ndani ndio wanaovuruga, si kwa sababu hawajui mema, bali kwa sababu hawataki mema yapatikane bila wao kuonekana kama vyanzo vyake.

Wengine wanatawaliwa na chuki, wivu, au tamaa ya madaraka. Wengine ni mateka wa ubinafsi, ukabila, udini, au mfumo dume unaowafanya waamini kuwa dunia inapaswa kuwaheshimu kwa jina, si kwa matendo.

Watu wa namna hiyo hawajui maana ya karma kuwa ni nguvu isiyoonekana ya matendo kurudi kwa mtendaji. Hawajui kwamba kila njama, kila uongo, kila usaliti, unajenga mzigo wa maumivu kwao wenyewe. Wanadanganyika na upepo wa muda mfupi wa umaarufu, bila kujua upepo huo huo unaweza kuwasomba kesho bila huruma.

Ndio maana, ninawasihi Watanzania wenzangu: tusiyumbishwe na wenye uchu wa madaraka, wale wanaoitumia mitandao kama uwanja wa chuki na uongo, wanaotafuta huruma kwa kueneza hofu. Tusikubali historia chafu za watu wachache ziandike upya mustakabali wetu.

Leo, tunayo nafasi ya kuchagua uongozi wa amani, utulivu, na maendeleo. Tunaye kiongozi anayetuonyesha kwa vitendo kwamba si maneno, bali matendo ndiyo yanayojenga taifa. Dkt. Samia Suluhu Hassan, mwanamke jasiri, kiongozi mwenye hekima na maono mapana. Ametuvusha katika majanga, ametengeneza fursa, ameweka Tanzania katika ramani ya dunia kwa umakini na utulivu.

Watanzania tusikwamishe kufanya maendeleo yetu wenyewe kwa tamaa na ujinga wa kubebeshwa na wenye uroho wa madaraka. Tutokeni tukapige kura kwa amani.

Tumchagueni kiongozi mwenye moyo wa kutuinulia uchumi wa nchi na wananchi, si kiongozi mwenye tamaa ya ubinafsi. Tukamchague Dkt. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Hussein Ally Mwinyi na wasaidizi wao.

Tukumbuke kuwa, tunapotoa hukumu, kupanga hila au kuendeleza fitna kwa maslahi binafsi, ni vyema tukatambua Mwamba (Mungu) anatuona. Ameshuhudia wapenda amani kote nchini wamemlilia juu ya amani, wamekesha kuwaombea viongozi wetu na kuliombea taifa letu.

Nawakumbusha kuwa, uongozi si kelele, ni utulivu. Si tamasha, ni huduma. Si ulafi, ni sadaka. Na mwisho wa yote, Mungu si mzee Mkumba, anaona, anasikia, na anapima kwa haki.

Mungu azidi kuwasamehe na kuwapuuza wale wachache wanaoongozwa na macho ya nyama badala ya hekima na utu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here