Kamwe usiwe kama Ronald Opus katika maisha yako

0
Forensic investigator working at a crime scene

Na Benny Benson

MACHI 23 mwaka 1994, tabibu mkaguzi (medical examiner) aliuchunguza mwili wa Ronald Opus na kufikia maamuzi kuwa, mtu huyo alikufa kwa kupigwa risasi kichwani. Hii inatokana na jeraha kubwa la risasi kichwani alilokutwa nalo marehemu.

Hapo ndipo tabibu mkaguzi pamoja na vyombo vya usalama wanakubaliana kuwa Ronald Opus hakujiangusha ghorofani kama ilivyodhaniwa hapo kabla, bali alipigwa risasi na kisha kuanguka au kuangushwa. Hivyo muuaji atafutwe.

Uchunguzi wa awali uliofanywa na vyombo vya usalama ulibaini kuwa, Opus alijirusha kutoka kwenye jengo la ghorofa kumi kwa lengo la kujiua huku akiwa ameacha kikaratasi chenye ujumbe mfupi wa maneno kwa yeyote atakayekisoma. Ujumbe kwenye kikaratasi hiyo ulisema; “Nasikitika/mnisamehe sana, siwezi kuwasamehe, nitakua kwa Mungu.”

Ilibainika kuwa, Ronald Opus alijirusha kutoka ghorofa ya kumi kwa lengo la kujiua, lakini akiwa ghorofa ya tisa wakati akidondoka chini, alipigwa risasi ya kichwani na mtu asiyefahamika kabla hajafika chini, hali iliyositisha maisha yake tangu akiwa angani.

Si marehemu Opus wala aliyefyatua risasi aliyekuwa akijua kuwa kwenye jengo lile kuliwekwa neti za usalama (safety nets) kwenye ghorofa ya nane kwa ajili ya kuwalinda waosha vioo wa ghorofa ya tisa na kumi wasidondoke chini iwapo itatokea ajali wakati wakisafisha vioo vya jengo.

Hizi neti za usalama huwa zinawekwa ili ikitokea mtu ameanguka, basi aangukie kwenye neti hizo na asipate madhara. Mwili wa marehemu ulikutwa juu ya neti ya usalama, kwa maana hiyo kilichomuua kijana huyo ni risasi aliyopigwa akiwa angani na si kingine. Kama isingekua risasi ile iliyomuua akiwa angani, basi dhamira yake ya kujiua isingetimia, maana zile neti zingemzuia kufika chini.

RISASI ILITOKA WAPI NA MUUAJI NI NANI?

Vyombo vya usalama vinaingia kazini, vinafanya uchunguzi wa kina (vetting) kwenye jengo lote na kubaini kuwa risasi iliyomuua Ronald Opus ilitoka kwenye chumba kilichopo ghorofa ya 9 ya jengo lile. Hii ni kutokana na kukutwa kwa ganda la risasi iliyotumika pamoja na tundu la risasi kwenye dirisha la moja ya vyumba vya ghorofa ya tisa kwenye jengo lile.

Chumba hicho anaishi mzee mmoja wa makamo pamoja na mke wake. Baada ya mahojiano marefu na mzee huyo, ikabainika alikuwa na ugomvi mkubwa wa kimahusiano na mke wake kwa muda mrefu. Ugomvi wao ukamfanya mzee yule kumtishia bunduki mke wake.

Mzee huyo alikuwa akitetemeka wakati ameshika bunduki. Ni kwasababu ya hasira kali aliyokuwa nayo, hivyo alishindwa kushika bunduki vizuri, hivyo alivyofyatua tu risasi ilimkosa mke wake na kupita dirishani kisha ikampata Opus aliyekuwa akidondoka kutoka ghorofa ya kumi katika harakati zake za kujiua.

SHERIA INASEMAJE?

Mtu ukiwa na lengo la kumuua mtu ‘A,’ lakini katika jaribio hilo kwa bahati mbaya ukamuua mtu ‘B,’ basi unakua hauna hatia ya kumuua mtu ‘B’. Hapa wana usalama wakaona wamepata muuaji wao, lakini utata ukazidi kuibuka. Mzee huyo nae akasema, hakuwa na nia ya kumuua mke wake bali alikuwa na lengo la kumtisha tu.

Anadai kuwa katika maisha yake yote huwa haachi risasi zikae ndani ya bunduki, hivyo anashangaa nani aliyeweka risasi ndani ya bunduki yake. Yeye mzee alifyatua akiwa na uhakika kabisa kuwa bunduki yake haikuwa na risasi hata moja.

Jambo hili linadhibitishwa na mke wake ambaye anadai mume wake amekua na tabia ya kumtishia kwa bunduki miaka nenda rudi katika ndoa yao kila wakikorofishana na hakuna siku hata moja risasi ilitoka kila alipoifyatua.

Uchunguzi zaidi unafanyika na kumuibua shahidi mwingine ambaye anadai kumtambua aliyeweka risasi ndani ya bastora ya mzee. Shahidi anasema, aliyeweka risasi hiyo ni kijana wa kiume wa huyo mzee wiki sita zilizopita. Shahidi anakiri kuwa alimuona kwa macho yake mwenyewe, lakini hakujua kama aliiweka kwa lengo gani.

Baadae ikabainika kwamba, mtoto huyo wa kiume alikua na uhasama mkubwa na mama yake ambaye aliamua kusitisha huduma zote za kifedha kwa mwanae. Mtoto huyo ikafika mahali akatamani kumuua mama yake. Ile tabia ya baba yake kumtishia mama yake bunduki ikatumika na huyu mtoto kama mwanya wa kumuua mama yake kupitia risasi moja aliyoiweka kwa siri, lengo kuu ikiwa ni kumuua mama yake kupitia mkono wa baba yake ambaye alizoea kumtishia mama ili baba akimtisha tena mama safari hii amuue kweli.

Katika hali ya kusikitisha ikafahamika kuwa mtoto huyo ndiye marehemu Ronald Opus. Ndiye mtoto wa wanandoa hawa. Risasi aliyoiweka kijana huyo kwenye bastola ya baba yake kwa lengo la kumuua mama yake, ndio imekatisha maisha yake mwenyewe.

Ronald baada ya kuona maisha yanakuwa magumu na mtego aliouweka ili mama yake apoteze maisha hautimii, aliamua kujiua yeye mwenyewe kwa kujitupa kutoka kwenye jengo walilokua wakiishi. Wakati akianguka kutoka ghorofa ya kumi, ndio muda ambao baba yake alifyatua risasi kumtishia mama yake.

Kwa bahati mbaya risasi ikamkosa mama sababu ya kutetemeka kwa mikono ya baba, hivyo risasi ikapita kwenye dirisha la chumba chao kilicho ghorofa ya tisa na kumpiga Ronald Opus ambaye alikuwa akianguka kutoka ghorofa ya kumi.

Kesi hii ilikuja kufungwa kama kesi ya kujiua (suicide) baada ya kuleta utata mkubwa katika maamuzi ya nani hasa mwenye hatia. Ronald Opus ni jina la muhusika kwenye kesi ya mauaji ya kufikirika ambayo imekuwa ikiripotiwa kama vile ni kesi ya kweli.

Kwa mara ya kwanza kesi hii ilisimuliwa na Don Harper Mills, kisha hapo baadae ikaja kusimuliwa na Rais wa Taasisi ya Sayansi ya Matukio tata ya Uhalifu huko Marekani. Don Harper Mills alisimulia kwenye hotuba wakati wa tafrija fulani mwaka 1987.

Ilipoanza tu kusambaa kama vile ni hadithi ya kweli na kisha kupata umaarufu mkubwa, watu wengi walimuona Don Mills (mtunzi) kama shujaa wa mahali hapo, lakini Mills akarudi kuuambia umma kuwa aliitunga hadithi hiyo ili kuonesha ni namna gani mara nyingine kesi za mauaji zinaweza kuwa zenye utata mkubwa.

Simulizi hii ilianza kusambaa kwa mara ya kwanza mwezi Agosti mwaka 1994. Ni kesi ya kutungwa tu ambayo iliitikisa dunia kwenye tovuti mbalimbali, kwenye ‘chat rooms’ hadi kwenye makaratasi mbalimbali (majarida, magazeti, vitabu nk). Vyombo vya habari vilivyokua vikiiripoti kesi hii, vilipokea zaidi ya barua 2000 na simu nyingi kutoka kwa watu mbalimbali duniani wakiomba kupewa kibali cha kuliweka tukio hili katika filamu.

Uzuri ni kwamba watu wote walioisimulia simulizi hii wakati huo hawakusahau kumtaja Don Mills ambaye ndiye mtunzi. Mills huiita ni ‘Simulizi ya ajabu’ na ameulizwa maswali mengi na watu wengi sana kwa miaka mingi kuhusu simulizi hiyo ya kufikirika. Baadhi ya vyombo vya habari, filamu na tamthilia zimewahi kutumia kisa hiki ambacho kina ujumbe mzuri.

Kwamba, tunatakiwa tusiwe na mikono mepesi katika kuandaa uovu ili kumdhuru mtu fulani. Wazungu husema “What goes around, comes around”. Kila mtu ana haki sawa ya kuishi aliyopewa na Mungu. Pamoja na dhambi zote tunazomfanyia Mungu, lakini bado ametupa nafasi ya kutubu, kusameheana wenyewe kwa wenyewe na kisha kuendelea na maisha. Wewe ni nani hata usiweze kusamehe?

Kuna watu ambao wanadhani uwepo wa watu fulani duniani ni wa bahati mbaya tu, hivyo hujipa Mamlaka ya kuwatendea uovu wowote ule wenzao na kusahau wema wote waliowahi kutendewa hapo kabla. Kuna watu hudhani kuwa watafanikiwa haraka kwa kumuua mtu fulani au kumshusha chini asifanikiwe kwa kutumia silaha za moto, unafiki, usaliti, uongo au uzushi na kusahau kuwa maisha ya kila mwanadamu yapo mikononi mwa Mwenyezi Mungu na ndiye muamuzi wa mwisho.

Tuna akina Ronald Opus wengi katika jamii. Kazi yao ni kuandaa uovu ili kuwashusha chini wengine kwa imani kuwa wao watainuka zaidi, lakini kwa bahati mbaya uovu huwarudia wao wenyewe. Nakusihi usiwe kama Ronald Opus katika maisha yako. Jifunze kusamehe na kusahau. Usilazimishe kupata rizki, Mungu atakupa tu kwa wakati na mahali muafaka, usichoke kumuomba na kumkumbusha kila wakati huku ukifanya kazi kwa bidii na maarifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here