KATIKA juhudi za kuboresha ustawi wa wanafunzi wa shule za msingi, Kampuni ya ATUZA imetoa msaada wa jozi 100 za viatu kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Miyombo iliyopo Kata ya Magindu, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.
Msaada huo umepokelewa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson John, katika hafla iliyofanyika ofisini kwake kabla ya kusambazwa kwa walengwa shuleni.

Akizungumza wakati wa makabidhiano, Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Bernadina Kahabuka, ameishukuru Kampuni ya ATUZA kwa mchango huo, akieleza kuwa kati ya wanafunzi 160 wa shule hiyo, 100 sasa watakuwa na viatu safi na bora.
“Huu ni msaada mkubwa kwa wanafunzi kutoka kaya zenye uhitaji. Tunawaomba wadau wengine waendelee kushirikiana nasi ili kuboresha mazingira ya elimu,” alisema.
Naye Diwani wa Kata ya Magindu na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Erasto Makaka, amepongeza juhudi hizo, akisema zinakwenda sambamba na azma ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha ustawi wa wanafunzi wa shule za msingi nchini.

Wananchi wa eneo hilo, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mbega, Moko, wameeleza kufurahishwa kwao na msaada huo, wakisema utawasaidia watoto wao kusoma katika mazingira bora.
Msaada wa viatu hivi umepokelewa kwa shukrani kubwa, huku ukitajwa kuwa suluhisho kwa changamoto ya wanafunzi wengi kutembea umbali mrefu kwenda shuleni wakiwa peku, hali inayoweza kuathiri afya na utendaji wao darasani.