HOSPITALI ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imeanza kambi maalum ya kutengeneza mishipa ya kuchuja damu sambamba na kupandikiza figo kwa wagonjwa wenye changamoto za figo ambayo itahitimishwa rasmi Julai 23, 2025.
Kambi hiyo inafanywa na wataalam wa Muhimbili Mloganzila kwa kushirikiana na jopo la wataalam kutoka Korea Kusini linalo ongozwa na Prof. Park Kwan Tae ambaye ni Daktari Bingwa Bobezi wa Upasuaji chini ya uaratibu wa Taasisi ya Africa Future Foundation (AFF) ya nchini Korea Kusini.
Upandikizaji wa figo unafanyika kwa kuvuna figo kutoka kwa mchangiaji kwa kutumia matundu madogo (Laparascopic Hand Assisted Donor Nephroctomy) utaalam ambao kwa hapa nchini unapatikana Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila pekee.
Aidha, wataalam mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi wanajengewa uwezo wa kutoa huduma hizo katika maeneo yao ili kuwapunguzia wananchi usumbufu wa kwenda mbali na maeneo yao kufuata huduma hizo.
Hadi kuhitimishwa kwa kambi hiyo wananchi takribani 60 watanufaika na huduma za kutengenezewa mishipa ya kuchuja damu na wananchi wanne watapandikizwa figo na kufikisha idadi ya wanufaika waliopandikizwa figo kufikia 19 tangu huduma hizo zilipoanza rasmi katika hospitali hiyo mwaka 2023.