Kamati ya bunge yaipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais

0

KAMATI ya kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imepongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa ubunifu mkubwa unaobeba uhalisia katika utekelezaji wa majukumu yake.

Pongezi hizo zimetolewa Machi 18, 2025 Bungeni Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Dkt. Joseph Mhagama wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa mpango na bajeti kwa mwaka 2024/2025 na makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi hiyo kwa mwaka 2025/2026.

Dkt. Mhagama alisema Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa ofisi ya mfano kwa sasa kutokana na kufanya kazi nzuri kutokana na watendaji wake kutekeleza maelekezo mbalimbali ya kamati na hivyo kuweza kupata matokeo makubwa katika kipindi kifupi.

“Wajumbe wa kamati hii tupo kwa zaidi ya miaka 10 sasa, lakini kwa kipindi hiki kifupi tumeshuhudia mageuzi makubwa ya kiutendaji katika utekelezaji wa majukumu ya ofisi hii, tunaomba tuendelee kushirikiana ili kufikia malengo,” alisema Mhagama.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni ameishukuru kamati hiyo kwa ushirikiano unaoendelea kuipatia ofisi hiyo na hivyo pongezi hizo zitakuwa chachu ya kufanya kazi nzuri zaidi.

“Hii ni kamati kubwa sana, kupokea pongezi hizi si jambo jepesi….hii inatupa faraja kuwa tunachokifanya kinaonekana na tuna ahidi kuongeza juhudi katika kutekeleza maelekezo mbalimbali yanayotolewa,” alisema Masauni.

Aidha, Masauni alisema Ofisi hiyo itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia ushauri na maoni ya kamati hiyo ili kufikia malengo iliyojiwekea.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here