Kama hili ni kweli, basi Chadema ni hatari kwa Taifa

0

KATIKA harakati za kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu, tunashuhudia mbinu zisizo za kawaida kutoka kwa baadhi ya vyama vya siasa vinavyotafuta uongozi kwa gharama yoyote.

Taarifa zilizotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (Itikadi, Uenezi, Siasa, na Mafunzo), CPA Amos Makala, zimefichua jambo la kutisha; ni madai kwamba Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinapanga kusambaza virusi vya Ebola na Mpox ili kuvuruga uchaguzi.

Ikiwa shutuma hizi ni za kweli, basi siasa ya upinzani inazidi kushuka hadhi na kugeuka kuwa tishio la moja kwa moja kwa afya ya wananchi na ustawi wa taifa kwa ujumla.

Taifa linahitaji viongozi wanaoamini katika demokrasia ya kweli, si wale wanaotafuta njia za giza kuhujumu mchakato wa uchaguzi kwa mbinu hatari kama hizi.

Katika historia ya siasa za upinzani nchini, mara kadhaa tumeshuhudia mikakati ya kueneza taharuki, kushawishi maandamano yasiyo na nidhamu, na hata kupinga taratibu halali za uchaguzi.

Lakini, kama sasa wanavuka mipaka kwa kupanga njama za kiafya, basi hatuna budi kusema wazi kuwa huu ni ubinafsi wa hali ya juu.

    Wananchi wanahitaji maendeleo, sera madhubuti, na siasa zenye tija, si wanasiasa wanaotumia njia za kutisha umma kwa magonjwa hatari ili kufanikisha malengo yao binafsi.

    SIASA ZINAZOPINGA UCHAGUZI NI UHUNI WA KIDEMOKRASIA

      Kwa muda mrefu, Chadema imejionyesha kama chama kinachopinga kila mchakato wa kidemokrasia nchini. Wamekuwa na historia ya kupinga matokeo ya chaguzi, kupinga Katiba inayosimamia mchakato wa uchaguzi, na hata kupinga maendeleo ya moja kwa moja kwa wananchi kwa visingizio mbalimbali.

      Sasa, ikiwa wanadaiwa kutumia hata njia za kibinadamu kama silaha za kisiasa, basi huu si upinzani wa kweli bali ni uhuni wa kisiasa. Chama chochote kinachopinga uchaguzi hakiwezi kuwa na dhamira ya demokrasia, na wananchi wanapaswa kuwa makini kutambua mbinu hizi.

      WANANCHI WATAKATAA NJAMA HIZI KWA KURA

        Hakuna taifa linaloweza kusonga mbele kwa siasa za njama na hila. Wananchi wanapaswa kufungua macho na kuelewa kuwa wapo wanasiasa wanaopenda giza na vurugu badala ya mwanga wa maendeleo.

        Katika uchaguzi ujao, kila Mtanzania anapaswa kufahamu kuwa kuna watu wasiotaka uchaguzi ufanyike kwa amani na wanajaribu kila njia kuhakikisha hilo halifanikiwi. Njia pekee ya kuwajibu ni kupitia kura, kuwaondoa kabisa kwenye uwanja wa kisiasa kwa kutumia haki ya kidemokrasia.

        TAIFA KWANZA, SIASA BAADAYE

        Kwa yeyote anayependa maendeleo ya nchi hii, shutuma hizi zinapaswa kuwa mwito wa tahadhari. Uchaguzi ni haki ya wananchi wote, na wale wanaotafuta mbinu za kuhujumu haki hii wanapaswa kusemwa wazi.

        Taifa linahitaji siasa safi, si siasa chafu zinazohatarisha uhai wa raia wake. Watanzania wanapaswa kuchagua maendeleo, si hofu!

        LEAVE A REPLY

        Please enter your comment!
        Please enter your name here