Na Iddy Mkwama
BABA wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwenye moja ya hotuba zake, aliwahi kusema, dhambi ya ubaguzi ni kama kula nyama ya mtu, ukila nyama ya mtu, utaendelea na hauwezi kuacha.
Mbali na maneno hayo, Mwalimu Nyerere katika kukemea vitendo vya ubaguzi, aliwahi kunukuliwa akisema, unapofika wakati wa uchaguzi, baadhi ya vyama au watu, wanaposhindwa kushawishi kwa kutumia sera wanatumia dini na ukabila.
Mwalimu Nyerere alisema, kutumia dini, ukabila au ukanda kwa ajili ya kupata madaraka, ni jambo linalowagawa.
Ukifuatilia kwa makini siasa anazofanya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Jussa Ismail Ladhu tangu wakati akiwa Chama cha Wananchi (CUF), utagundua kwamba, ametawaliwa na dhambi ya ubaguzi.
Jussa, hivisasa suala la kutoa matamshi yenye viashiria vya ubaguzi, ni kawaida kwake, ni kama moja ya mavazi ambayo mwenyewe anaona yanampendeza, lakini hayaleti picha nzuri kwenye jamii.
Hata hivyo, ukitazama kwa kina sababu za Jussa kufanya yote hayo, ni kutaka kueneza chuki dhidi ya kundi fulani, ili kukipa nguvu chama chake, lakini ukweli ni kwamba, siasa za aina hiyo hazimsaidii yeye wala chama chake; badala yake anakidhoofisha.
Ukizungumza na Wazanzibar hivisasa, vinywa vyao vimetawaliwa na siasa safi na pongezi za hatua kubwa ya maendeleo ambayo imepigwa chini ya uongozi wa Rais wa Awamu ya Nane Dkt. Hussein Mwinyi.
Wazanzibar hawataki tena kusikia siasa za utengano na chuki ambazo zimewapotezea muda mwingi. Hawataki kukumbuka enzi zile walizochochewa na wanasiasa wenye uchu wa madaraka ambao walitumia damu za ndugu zao ili washike dola.
Hawataki siasa ambazo ziliwafanya washindwe kuzikana wala kujuliana hali. Ni siasa ambazo ziliwafikisha hatua ambayo huduma au bidhaa zilinunuliwa au kutolewa kwa kuangalia itikadi za vyama.
Miaka kadhaa nyuma, niliwahi kufanya ziara visiwani Pemba, nilitamani kufika Kisiwa Panza ambako niliwahi kusikia simulizi nyingi ambazo nilitaka kwenda kujua ukweli wake.
Nikiwa upande wa pili wa kisiwa hicho, nilikuta mzozo mkubwa, nikauliza sababu ya mzozo huo, nikaambiwa kwamba, kivuko kinamilikiwa na mwanachama wa CUF, kwahiyo wanaoruhusiwa kuvuka ni watu wenye itikadi ya chama hicho tu, wengine wanunue vivuko vyao!
Siku hiyo idadi kubwa ya waliotaka kuvuka walikuwa ni wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), hivyo chombo hicho kiligoma kufanya safari zake.
Kwa maana hiyo, ndoto yangu ya kwenda kusikia simulizi za Kisiwa hicho zikaishia hapo kwasababu ya siasa za ubaguzi ambazo zilishamiri kwa miaka hiyo, lakini sasa Zanzibar ni shwari!
Kwa kiasi kikubwa, walioifikisha Zanzibar kwenye siasa za aina hiyo, ni Jussa na kundi lake, wakati huo akiwa CUF na baada ya Wazanzibar kuzichoka siasa hizo, chama hicho kilipoteza nguvu kubwa Kisiwani humo na sasa anaendelea siasa zile zile akiwa ACT.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa, moja ya kauli mbaya na zilizochochea chuki, ni ile iliyowahi kutolewa na Juma Duni Haji mwaka 1995 kwenye uwanja wa Kibandamaiti na kudai mwaka huo ndiyo mwisho wa utawala wa mtu mweusi.
Naye Jussa kwenye mkutano huo huo, alinukuliwa akisema CCM ilishinda uchaguzi mdogo wa jimbo Uzini kutokana na kuwepo Wabara pamoja na Wakristo, maneno ambayo yalionyesha wazi nia ovu ya viongozi hao.
Nakumbuka Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya CUF Mussa Haji Kombo miaka kadhaa iliyopita, aliwahi kuonya kuhusu mwenendo usioridhisha wa viongozi wa chama hicho, akasema iwapo chama hicho hakitabadilisha kasoro zake za kimsingi na kuwapiga marufuku viongozi wasiojua siasa ambao huropoka majukwaani, wananchi wengi watakichoka chama hicho.
Kombo akinukuliwa na chombo kimoja cha habari nchini alisema, wakati Duni akiwa mgombea mwenza wa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Prof. Ibrahim Lipumba, katika uchaguzi wa kwanza mwaka 1995, alitumwa na mmoja wa viongozi wake aseme ‘utawala wa mtu mweusi umefika tamati Zanzibar.’
Alisema, mara baada ya matamshi hayo hali ya hewa kisiasa katika visiwa vya Zanzibar na Muungano zilichafuka ghafla, huku CUF kikishindwa jinsi ya kujieleza kutokana na uzito wa matamshi hayo ambayo yalileta mkanganyiko ndani na nje ya Zanzibar.
“Duni na Jussa wamekipata athari isiyosahaulika chama chetu. Huwezi kusema utawala wa muafrika umefika mwisho wakati wewe kimuonekano ni muafrika halisi. Bila shaka utakuwa umetumwa useme hivyo ili kuwathibitishia wapiga kura chama chenu ni wakala aidha wa Waarabu au Wazungu,” alisema Kombo.
Alisema, hata msimamo wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF wakati huo Maalim Seif Shariff Hamad kutaka Muungano wa mkataba kinyume na sera ya chama hicho, ilikuwa ni ajenda yake yenye lengo la kuligawa Taifa.
“Kama ni mwanasiasa au kiongozi mwenye upeo wa kisasa yakupasa utambue Ukristo na Wakristo hawatakwisha duniani. Uislamu na Waislamu hawatamalizika ulimwenguni. Wabara na Wazanzibar tayari wamechanganya damu na hawatatenganishwa kwa utawala na siasa. Kuutaja ubara au udini ni kufilisika kisiasa,” alinukuliwa Kombo.
Kombo akionekana kumshangaa Duni, alisema kwa mwanasiasa mwenye kiwango cha elimu kama Duni, kisha akakubali kulishwa maneno na kutamka usaliti dhidi ya Waafrika wenzake, imetosha kuthibitisha kuwa maarifa yake katika siasa na uongozi ni mafupi yasiyojitosheleza.
“Idadi kubwa ya Wazanzibari ndiyo waliojijenga Tanzania Bara kwa kujenga nyumba, kuanzisha miradi, mashamba, mitaji na miradi. Ni vyema kudai Muungano uwepo Muungano wa Serikali tatu wa haki, wenye usawa na heshima ila si kujenga fikra ya kuvunja Muungano,” alisema Mwanasiasa huyo.
Alisema, hata Duni alipohama CUF kwenda Chadema kwa tamaa ya kushika madaraka ya umakamo wa Rais au kupata fedha, hakumshangaa kwasababu alizodai kama aliweza kuwasaliti Waafrika wenzake kwa kuwatamani wakoloni warejee, asingeshindwa kuuuzwa Chadema kwa mkopo.
“Matamshi ya kina Duni na Jussa mara kadhaa yamekuwa hayaonyeshi taswira na kulinda umoja wa Kitaifa na kuonekana kama wanasiasa wenye maagizo au waliopewa mradi wa kuligawa Taifa.”
“Hakuna Mzanzibari mwenye nyumba miradi, mashamba na biashara Tanzania Bara atakayekubali kuwasikiliza wasiotaka Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Watawaitikia midomoni mwao ila wakati wa kupiga kura watakakataa kwa ajili ya kulinda maslahi yao kiuchumi,” alinukuliwa Kombo.
Zipo kauli nyingi ambazo zinaonyesha wazi kwamba, Jussa ni mbaguzi na anapaswa kupuuzwa kama ambavyo Wazanzibar walivyoamua kumpuuza na kumuunga mkono Rais Dkt. Hussein Mwinyi ambaye tangu alipoingia madarakani, amefanya mambo makubwa.
Naamini, kelele wanazopiga ACT hivisasa visiwani Zanzibar, ni dalili za kushindwa kabla ya Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoka mwaka huu.
Jussa na viongozi wenzake baada ya kuona hawatakuwa na jambo lolote la kuwaeleza Wazanzibar ili wachaguliwe, wameamua kufanya siasa za ubaguzi kwa ajili ya kuwagawa Wazanzibar; siasa ambazo zimepitwa na wakati na zitakipoteza chama hicho kwenye ramani ya kisiasa.
Mwanasiasa huyo anapaswa kusoma alama za nyakati na kusoma fikra za wananchi wa visiwa hivyo ambao wanahitaji maendeleo yanayoonekana na ni dhahiri hakuna haja ya kutafuta tochi au darubini ili kuyaona; yanaonekana kwa macho ya kawaida.
Hakika, Rais Dkt. Hussein Mwinyi baada ya kupitishwa kuwa mgombea Urais kwenye mkutano maalum wa Chama cha Mapinduzi CCM, uliofanyika hivi karibuni jijini Dodoma, ataingia kwenye uchaguzi ujao akiwa na mtaji mkubwa wa mambo aliyoyafanya kwa Awamu ya Kwanza ya urais na atashinda kwa kishindo.