Jiji la Mwanza lapata mwarobaini wa msongamano wa magari

0

UJENZI wa Barabara ya Buhongwa-Igoma yenye urefu wa KM 14 kwa kiwango cha lami inayojengwa katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza inatajwa kuwa ndio mwarobaini wa changamoto ya msongamano wa magari jijini humo.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Wakili Kiomoni Kibamba wakati akielezea hali ya utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Jiji la Mwanza kupitia Mradi wa Uendelezaji Miji na Majiji Tanzania (TACTIC) na manufaa yake kwa wananchi.

Alisema, barabara hiyo inayounganisha Kata nne ambazo ni Buhongwa, Lwanhima, Kishiri na Igoma ilikuwa na changamoto kubwa hali iliyopelekea magari yote yaliyokuwa yakitoka Buhongwa kwenda Igoma au Igoma kwenda Buhongwa kulazimika kuingia katikati ya jiji hivyo kuongeza msongamano wa magari.

Wakili Kibamba ameongeza kuwa ujenzi wa barabara hiyo utasaidia kupunguza msongamano huo kwa kiasi kikubwa kwani magari yote yaliyokuwa yanatoka maeneo hayo hayatolazimika kuingia katikati ya Jiji badala yake yatakwenda moja kwa moja ama Igoma au Buhongwa.

Vilevile, Mradi wa (TACTIC) katika Jiji la Mwanza unatekeleza Mradi wa ujenzi wa Soko la samaki wabichi Kata ya Mkuyuni ambapo kwa mujibu wa Wakili Kibamba amesema kuwa hiyo ilikuwa ni changamoto iliyokuwa inawakabili kwa muda mrefu.

“Halmashauri ya Jiji la Mwanza tulikuwa na changamoto ya kukosekana kwa eneo la kuuzia mazao ya uvuvi. Ujenzi wa soko la samaki la Mkuyuni litawezesha kunyanyua uchumi kwa sababu hata haya maboti ya uvuvi yanayotoka Wilaya ya Ukerewe na upande wa Buchosa Wilayani Sengerema yatakuwa yanakuja kuuzia samaki kwenye soko hili, kwa hiyo tutafungua uchumi sio wa hapa tu lakini pia imesaidia mazingira ya uwezeshaji wa kufanya biashara kati ya Mwanza na Mikoa mingine” amebainisha Wakili Kibamba

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here