Jeshi la Polisi latakiwa kuimarisha ushirikiano na wadau

0

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amesema ni muhimu Jeshi la Polisi kuimarisha ushirikiano wa karibu na wadau wote wa uchaguzi, hatua ambayo itasaidia kuhakikisha kila mdau anatendewa haki, na kuondoa tofauti zinazoweza kusababisha migongano.

Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi unaofanyika katika ukumbi wa Chuo Cha Polisi (CCP) Moshi Mkoani Kilimanjaro.

Alisema, baadhi ya maeneo muhimu ya ushirikiano ni pamoja na kuhakikisha mikutano ya kampeni inafanyika kwenye maeneo yaliyoruhusiwa na ndani ya muda uliopangwa, Kuzuia maandamano yasiyo na kibali, kuimarisha ulinzi wa wagombea na viongozi wa vyama vya kisiasa, bila kujali vyama vyao au itikadi zao pamoja na kudhibiti misongamano mikubwa ya watu ili kuhakikisha shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi zinaendelea bila usumbufu.

Pia, Makamu wa Rais amelitaka Jeshi la Polisi kushirikiana kwa karibu na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) pamoja na taasisi nyingine za Serikali ili kujiandaa vyema kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kufuatilia taarifa mbalimbali zenye mlengo wa uchochezi, zinazotolewa kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vingine vya habari.

Alisema, kwa kutumia teknolojia za akili bandia baadhi ya watu wanaweza kusambaza picha au video za uongo za wagombea wa vyama vya siasa, jambo linaloweza kuleta madhara makubwa kwa amani na utulivu wa jamii.

Makamu wa Rais alisema, Jeshi la Polisi linapaswa kujiandaa kikamilifu kufanya doria ya mtandao ili kubaini na kuchambua machapisho, picha, na video zenye viashiria vya uvunjifu wa sheria, na kuchukua hatua za kisheria kwa haraka.

Vilevile, Makamu wa Rais amesisitiza Jeshi la Polisi lishirikiane kwa karibu na wadau wengine wa uchaguzi, ikiwemo TAKUKURU na vyombo vingine vya usalama, ili kudhibiti vitendo vya Rushwa katika kipindi cha uchaguzi.

Aliongeza kwamba, ni muhimu Jeshi la Polisi likijumuisha Polisi Jamii lishirikiane kwa karibu na TAMISEMI katika kusimamia usalama, hasa katika ngazi za Kata, Shehia, Vijiji na Mitaa.

Makamu wa Rais amelitaka Jeshi la Polisi kusimamia vema utekelezaji wa sheria ya uchaguzi na sheria nyingine za nchi.

Alisema, ni wajibu wa Jeshi la Polisi na wadau wengine wa uchaguzi, kuielewa vizuri Sheria ya Uchaguzi na kusimamia utekelezaji wake, ili kuepuka kuonea watu na kuvuruga uchaguzi.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi na viongozi wa vyama vya siasa kuepuka kujichukulia sheria mkononi pale wanapoona ukiukwaji wa sheria za uchaguzi, na badala yake watoe taarifa kwenye vyombo vya sheria kwa hatua stahiki.

Halikadhalika Makamu wa Rais alisema, katika kuelekea Uchaguzi Mkuu ni muhimu kuendelea kuwajengea uwezo maafisa na askari kwa kuwapatia mafunzo ya utayari, uadilifu, na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Amempongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi kwa kuendelea kuhakikisha askari wa Jeshi la Polisi wanapata mafunzo ya kitaalam ya kuwajengea uwezo na utayari.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Daniel Sillo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Wizara kibajeti,vifaa na vitendea kazi vya kisasa ambavyo vimesaidia kuimarisha na kuboresha utendaji wa Jeshi la Polisi na vyombo vya usalama vilivyopo chini ya Wizara hiyo.

Ameishukuru Serikali kwa kutoa vibali vya ajira na upandishaji vyeo hali inayosaidia katika udhibiti wa uhalifu nchini na kuongeza ari ya utendaji kazi kwa maafisa na askari ndani ya Wizara.

Alisema, Wizara na vyombo vyote vya usalama vilivyo chini yake itaendelea kufanya kazi kwa ushirikiano, nidhamu, weledi na uadilifu ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama yenye amani na utulivu na mazingira mazuri kwa ajili maendeleo na uchumi endelevu wa Taifa.

Awali, akitoa taarifa ya Mkutano huo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Camillus Wambura amesema Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu na kuwasihi Watanzania wawe na uhakika na utulivu wakiamini kipindi hicho chote kitapita katika hali ya usalama na utulivu wa hali ya juu pamoja na Serikali itakayochaguliwa itaingia madarakani bila kikwazo.

Alisema, kauli mbiu inayoongoza mkutano huo inaweka msisitizo katika kusimamia amani na utulivu wakati wote wa mchakato wa uchaguzi ili kuhakikisha wananchi wanashiriki kwa utulivu, uhuru na amani bila kuwa na vikwazo vya aina yeyote.

Pia, alisema inasisitiza na kuweka jukumu kwa kila mwananchi kuhakikisha analinda amani usalama na utulivu kipindi cha kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Mkutano huo wa siku tano kuanzia tarehe 11-15 Agosti 2025 unaongozwa na kauli mbiu isemayo “Amani, Utulivu na Usalama kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu 2025 ni jukumu letu sote”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here