JAPAN kununua Kilo Milioni 30 za tumbaku ya wakulima wa Tanzania

0
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana Rais na Mtendaji Mkuu wa Japan Tobacco International (JTI) Bw. Masamichi Terabatake, baada ya kikao kilichofanyika katika ofisi hiyo, iliyopo Kamiacho, jijini Tokyo Japan, Septemba 26.2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

“Leo Bodi ya Wakurugenzi imetangaza uamuzi wa kununua Kilo Milioni 30 za tumbaku kutoka kilo milioni 14 ambazo walinunua msimu uliopita. Hii ni fursa kubwa kwa wakulima wetu kwani kiasi hicho ni zaidi ya uzalishaji wa zao la tumbaku Tanzania,”

KAMPUNI ya Japan Tobacco Incorporation (JTI) imeahidi kununua Kilo Milioni 30 za tumbaku kutoka kwa wakulima wa Tanzania katika msimu ujao wa kilimo.

Ahadi hiyo imetolewa na Rais na Mtendaji Mkuu wa JTI, Masamichi Terabatake mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyetembelea ofisi zao ili kuwahakikishia utekelezaji wa mazungumzo yaliyofanyika wakati wa mkutano wa TICAD 8, jijini Tunis, Agosti, mwaka huu.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Waziri Mkuu amesema uamuzi wa kampuni hiyo kuongeza kiwango cha ununuzi wa tumbaku utatoa ahueni kwa wakulima wa Tanzania ambao walikuwa hawana uhakika wa soko la zao hilo.

“Leo Bodi ya Wakurugenzi imetangaza uamuzi wa kununua Kilo Milioni 30 za tumbaku kutoka kilo milioni 14 ambazo walinunua msimu uliopita. Hii ni fursa kubwa kwa wakulima wetu kwani kiasi hicho ni zaidi ya uzalishaji wa zao la tumbaku Tanzania,” alisema.

“Miaka ya nyuma makampuni yaliyokuwa yakinunua tumbaku yalizoea kuwapangia wakulima wetu idadi ya kilo za kununua, kwa hiyo hata uzalishaji haukuwa mkubwa sana. Nikiwa ziarani Tabora, nilikutana na viongozi wakuu wa vyama vya wakulima wa zao hili, na waliomba kupewa fursa ya kuongeza soko, kwa hiyo wakulima sasa waongeze uzalishaji ili tufikie lengo hili,” alisisitiza.

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na Mwenyekiti wa Bodi ya JTI, Mutsuo Iwai na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC), Takashi Araki. Waziri Mkuu yuko Japan akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mazishi ya Waziri Mkuu mstaafu wa nchi hiyo, Shinzo Abe yanayotarajia kufanyika kesho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here